MFANYAKAZI wa kazi za ndani mwanaume,Yasin Abdala (35), Kitongoji cha Kivungwi Kwazoka ,Kata ya Vigwaza Chalinze,Bagamoyo mkoani Pwani ameuwawa na wananchi wenye hasira kali baada kuwauwa watoto wawili wa bosi wake ,kwa kuwakatakata mapanga.
Aidha marehemu pia amemjeruhi mama wa watoto hao Sada Salehe (28) kwa kumshambulia sehemu mbalimbali za mwili na kukimbizwa kituo cha afya Mlandizi kwa matibabu zaidi
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kamanda wa polisi mkoani Pwani Wankyo Nyigesa alieleza ,tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Julai 9 nyumbani kwa Wema Senzie.
Alisema, mtuhumiwa ameuwawa na wananchi waliokwenda kumkamata baada ya kukimbia alipokuwa amehifadhiwa kwenye ofisi ya Kijiji.
Wankyo ,aliwataja Watoto hao aliowaua ni Abubakary Makolo (6) mwanafunzi wa darasa la kwanza shule ya msingi Kwazoka na mdogo wake Rehema Makolo (5) mwanafunzi wa shule ya awali Kwazoka.
“Mtuhumiwa baada ya kukamatwa alihifadhiwa ofisini hapo kwa ajili ya kupelekwa kwenye vyombo vya sheria lakini alivunja mlango na kukimbia na walipomkamata walimshambulia kwa silaha za jadi na kusababisha kifo chake,” alisema Wankyo.
Wankyo alibainisha, chanzo cha mauaji hayo kinachunguzwa na polisi ila awali kabla ya tukio hilo mtuhumiwa alikuwa na ugomvi na mama wa watoto hao.
Miili ya marehemu imehifadhiwa kwenye kituo cha afya Mlandizi ,kusubiri taratibu za mazishi.
Post A Comment: