NA MWANDISHI WETU

MDAU wa Maendeleo Wilaya ya Busega ambaye pia ni Kada wa Chama Cha Mapinduzi CCM, Joseph Goryo 'Muddy'  ameongoza kura za maoni Udiwani Kata ya Lamadi,baada ya kupata kura 43 huku mshindi wa Pili Emanuel Desela akipata kura 34 na wa tatu,Martine Buberwa akipata kura 31.

Zoezi hilo la kura za maoni ziliendeshwa na Katibu wa CCM, Kata ya Lamadi, George Batondo na kusimamiwa na Mkuu wa Wilaya ya Busega, Bi. Tano Mwera ambaye alitangaza matokeo hayo kuanzia mshindi wa kwanza hadi wa mwisho.

Awali akinadi sera zake katika zoezi hilo la kuomba kupigiwa kura kwa Wajumbe wa Kata hiyo, aliahidi endapp atapata nafas, atahakikisha vipaumbele muhimu vinafanyiwa kazi kwa kushirikiana na ngazi zote za Serikali pamoja na wadau  wa ndani na wale wa nje.                                     
Goryo alisema lengo ni kuhakikisha Lamadi inafikia malengo yake ya kimaendeleo ikiwemo ya miundombinu kama barabara za mitaa ya Kata hiyo, ujenzi wa Stendi kubwa ya kisasa ya mabasi Mji wa Lamadi, miundombinu ya maji safi,ujenzi shule za sekondari na madarasa ya sekondari kwa Wanafunzi wanaoongezeka kila mwaka.

"Namshukuru Mungu kwa hatua hii. Lakini pia Wajumbe walioonesha imani kwangu na kunipigia kura ndani ya Chama hii ni heshima tosha na ya kipekee hakika tuendelee kumuomba Mungu.

"Tunahitaji kuona safari ya Lamadi mpya yenye maendeleo ya kisasa inatimia.

Lamadi ni mlango wa uchumi. Nitatumia fursa zilizopo kuhakikisha Wananchi wa Lamadi wananufaika na Uchumi uliopo ndani ya Kata yao ili uwaletee maendeleo" alisema Goryo.

"Lamadi yenye Maendeleo imara inawezekana. Tutahakikisha tunahimalisha miundombinu mto Lamadi ili kukabiriana na mafuriko yanayojaa mara kwa mara eneo la Soko la Kisesa na maeneo ya Lamadi.

"Tutajenga kituo cha Mabasi kikubwa na cha kisasa kitaongeza ajira katika mji wetu" alisema Goryo

Katika suala la elimu, Goryo alisema watahakikisha wanaongeza shule zaidi za sekondari pamoja na ujenzi wa madarasa kwa wanaoanza kidato cha kwanza.

"Nitakapopata nafasi ya kupeperusha bendera ya CCM, tutapata ushindi wa kishindo kura nyingi za Urais, Ubunge na Udiwani,...nitahakikisha tunafanikisha kusajiri shule ya sekondari na pia ujenzi wa madarasa.

Lakini pia suala la maji safi tutahakikisha tunalipigania na maeneo ya Kata ya Lamadi yaliyopitiwa na miradi ya maji inanufaika na maji safi." Alisema Goryo.

Aidha, Goryo aliomba Wana-Lamadi kuendelea kumpa ushikirikiano na  kumuombea hatua inayofuata ndani ya chama.

Katika hatua nyingine, Goryo alitoa salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Wiliam Mkapa, aliyefariki  dunia usiku wa Ijumaa ya 23 Julai mwaka huu.                 
"Wana-Lamadi tumepokea kwa  masikitiko kifo cha mpendwa wetu Mzee Mkapa. Watanzania tuendelee kuungana na mshikamano kwa kuyakimbilia yale yote aliyotuachia" Alisema Goryo.

Goryo alimalizia kuwa, katika kuhakikisha anatimiza ndoto yake, atahakikisha anajenga shule ya ufundi ndani ya Kata hiyo kwa lengo la kusaidia vijana waliomaliza darasa la Saba na  walioshindwa kujiendeleza elimu ya sekondari.

"Nina maono ya kuanzisha shule ya ufundi ambayo itakuwa ni kwa ajili ya watoto wanaomaliza darasa la Saba ili waweze kusoma bure katika shule hiyo itakayokuwa ya ufundi na ushonaji" Alimalizia Goryo.

Goryo ambaye pia ni mkulima na mfugaji wa kisasa, amekuwa mdau mkubwa wa kusaidia jamii ya watu mbalimbali wakiwemo watoto wenye mahitaji maalum ndani ya Mkoa wa Simiyu na mikoa mingine ambapo anaamini kwa sasa ni muda muafaka kushawishi wale marafiki waliokuwa wakisaidia kusaidia waje sasa kuwekeza Lamadi.

 Mwisho
Share To:

Post A Comment: