Mbunge wa Jimbo la Ilemela ambae pia ni Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Dkt Angeline Mabula amewasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo zilizoahidiwa na Chama Cha Mapinduzi kupitia Ilani yake ya Uchaguzi kwa kipindi cha 2015-2020 kwa wajumbe wa halmashauri kuu ya chama hicho kwa wilaya ya Ilemela.

Akizungumza wakati wa uwasilishaji wa taarifa hiyo, Mbunge Dkt Mabula amesema kuwa katika sekta ya elimu Jimbo la Ilemela limeendelea kuwa kinara kwa kushika nafasi ya kwanza kimkoa kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo mpaka sasa sanjari na kuwa ndani ya kumi bora kwa kipindi chote, huku shule mpya sita zikijengwa tatu zikiwa za elimu msingi(Bezi, Kayenze ndogo na Ihalalo) na tatu nyengine za sekondari(Kayenze, Angeline Mabula na Kisundi) sambamba na kuwashukuru wananchi na wadau kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kumaliza tatizo la upungufu wa madawati na vyumba vya madarasa ambapo harambee ya uchangiaji wa shughuli za maendeleo ilifanyika mapema baada ya kuingia madarakani iliyosaidia kutatua changamoto ya upungufu wa miundombinu ya kujifunzia na kufundishia, Wakati katika sekta ya mapato jimbo hilo likiweza kukusanya zaidi ya 92% ya mapato ya ndani mpaka sasa ukilinganisha na lengo lilikuwa linekusudiw hapo awali.

'.. Moja ya mradi unaonipa raha kwa kweli ni kile kivuko cha Kayenze kuelekea Bezi, Nasikia sasa hivi kinaenda mpaka ukerewe na juzi tulikuwa tunaongea na mkurugenzi mkuu wa TEMESA tuone namna ya kuongeza kivuko kingine ili viweze kupishana ..' Alisema

Aidha Mhe Dkt Mabula ametaja mafanikio yaliyofikiwa katika sekta ya afya ikiwemo ujenzi wa hospitali mpya ya wilaya, vituo vya afya (Karume, Buzuruga), upatikanaji wa dawa muhimu, mapambano dhidi ya malaria na Ukimwi, huduma kwa wazee na watu wenye ulemavu, Katika sekta ya Ardhi jimbo hilo likiongoza katika zoezi la urasimishaji wa makazi kwa miaka miwili mfululizo ambapo hati 10,772 zimeandaliwa mpaka sasa, viwanja 68,000 vimebuniwa na viwanja 83,352 vikipimwa, Migogoro ya muda mrefu ya Ardhi imepatiwa ufumbuzi ikiwemo ule wa Nyagunguru ambapo Serikali ilishafanya uthamini na uhakiki na kulipa fidia ya shilingi 3,534,295,165.58, Mgogoro wa Jeshi la Wananchi JWTZ na wananchi wa kata ya Kahama uthamini ukifanyika na uhakiki unaendelea na jumla ya shilingi 6,195,133,000.00 zikitegemewa kulipwa fidia, Mgogoro wa eneo la Kigoto kati ya wananchi na jeshi la polisi ukimalizwa kwa wananchi kurasimishiwa maeneo yao na polisi kubaki na eneo lililosalia.
Sekta ya Maji miradi ya zaidi ya kiasi cha Euro milioni 104.5 imetekelezwa ikiwemo ujenzi wa tanki la maji Nyasaka, Kitangiri, ujenzi wa visima vya maji kwa ushirikiano wa mufti mkuu wa Tanzania na  mradi wa visima 10 vijijini.
 
Wakati katika sekta ya miundombinu mradi wa Barabara ya kutoka Sabasaba-Kiseke-Buswelu ukikamilika, barabara ya Nyakato steel-Buswelu ikikaribia kukamiliza sanjari na kufungua barabara kale za kipindi cha mkoloni ilizokuwa hazipitiki kwa fedha za mfuko wa jimbo, Huku utoaji wa mikopo ya halmashauri  na uwezeshaji wananchi kiuchumi kupitia taasisi za kifedha na wadau wengine kukishika kasi.

Akifungua kikao hicho mwenyekiti wa CCM wilaya ya Ilemela Mhe Nelson Mesha mbali na kupokea taarifa iliyowasilishwa, Akatahadharisha wajumbe wa kikao hicho juu ya kutenda haki kwa wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi  kwani hao ndio viongozi wanaotegemewa na kuacha kutoa nje siri za vikao jambo linalochangia uwepo wa makundi ya uchaguzi, chuki na taharuki kwa wanachama.

Akihitimisha katibu wa CCM wilayani humo, Bi Aziza Isimbula amempongeza mbunge wa jimbo hilo kwa utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi kwani hatua hiyo itakisaidia chama kupata ushindi katika uchaguzi mkuu ujao sambamba na kutoa wito kwa wanachama hao kujitokeza kuchukua fomu za uongozi wa nafasi za udiwani na ubunge kuanzia Julai 14-17, 2020 huku akiwaasa kuzingatia kanuni, katiba ya CCM na taratibu nyengine za uchaguzi ili zoezi hilo liweze kukamilika kwa ufanisi.
Share To:

Post A Comment: