NA TIGANYA VINCENT, TABORA.
MKUU wa Mkoa wa Tabora Dkt. Philemon Sengati amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Nzega Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP) Advera Bulimba kuhakikisha anakomesha vitendo vya mauaji vinavyotokana na wananchi kujichukulia Sheria mikononi.

Ametoa agizo hilo jana mara baada ya kumuapisha Mkuu huyo mpya wa Wilaya ya Nzega anayekwenda kushika nafasi ya Godfley Ngupula.

Alisema Wilaya hiyo inakabiliwa na tatizo la baadhi wa watu kuamua kuwaua wenzao kwa imani za kishirikina na wivu wa kimapenzi , jambo linalotia doa Mkoa.

“Nenda ukatumie ukatumie uzoefu wako na mafunzo na ujuzi ulionao ukakomesha tabia ya baadhi ya watu kuamua kukatisha maisha ya wenzao…mkashirikiane na viongozi wenzao kuhakikisha tatizo hilo linakwisha na wananchi wote wanaishi kwa Amani”alisema.

Alisema ni vema wakahakikisha wanasimamia haki na kufanyakazi kwa usawa ili wanyonge wanoanyanyaswa wapate kilimbilio na kupata majawabu ya kero zao ili Wilaya hiyo iwe mfano kwa Mkoa wa Tabora.

Dkt. Sengati alimtaka kuhakikisha anasimamia watumishi waliochini yake katika kujenga uchumi wa Wilaya ya Nzega na kuimarisha upatikanaji huduma bora kwa wananchi hasa kwa wale wanaoishi pembezeni.

“Nenda ukachape kazi ili uweze kuacha alama kama kielelezo cha utendaji wake kwa wananchi” alisema

Aidha Mkuu huyo wa Mkoa wa Tabora aliwataka vijana walioteliwa kushika nafasi mbalimbali kuhakikisha wanafanyakazi kwa uzalendo na uadilifu ili kumwonyesha Mhe. Rais kuwa hakukosea kuwaamini.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Nzega Kamishina Msaidizi wa polisi Bulimba alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kumwamini na kuweza kumteua kushika nafasi hiyo ya uongozi.

Aliahidi  kuchapa kazi ya kuwatumikia wananchi kwa haki na usawa bila ya upendeleo ili kumwakilisha Rais ipasavyo katika Wilaya hiyo.

ACP Bulimba aliwataka kushirikiana katika kuhakikisha wanatatua matatizo ya wananchi ili waweze kufikia malengo yao.

Mkuu huyo wa Wilaya ya Nzega aliteuliwa hivi karibuni kuchukua nafasi ya mtangulizi wake Godfrey Ngupula ambaye amestaafu
Share To:

Post A Comment: