Na Mwandishi
Wetu, Mwanza
Katibu MKuu
wa Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi ameutaka
uongozi wa Chuo cha Michezo Malya kuongeza ubunifu katika aina ya mafunzo
yanayotolewa na chuo hicho.
Akiwa
ziarani Chuoni hapo, jana tarehe 7 Juni,2020 Dkt Abbasi ambaye pia ni
Msemaji Mkuu wa Serikali, alishangazwa na Chuo hicho kuwa na wataalamu
mbalimbali wa michezo lakini hakuna wataalamu kutoka chuo hicho katika soko la
michezo hasa ligi mbalimbali nchini.
"Nafahamu
mmekuwa mkijikita zaidi kuzalisha maafisa michezo, hilo mnapaswa kwenda zaidi
ya hapo kwa sasa. Lazima pia mjibu mahitaji ya soko la michezo nchini,"
alisema Dkt. Abbasi.
Alikiagiza
Chuo hicho kuboresha mitaala yake ili kikidhi mahitaji ya soko hasa la sekta
binafsi ikiwemo kuzalisha wataalamu kama makocha, wasemaji wa vilabu, wasimamia
masuala ya vifaa na ufundi na watendaji wengine.
"Historia
ya Chuo hiki imesheheni maono ya Baba wa Taifa tangu miaka ya 1970
kilipoasisiwa. Maoni hayo yanaishi hata sasa na tunapaswa kufikiria kwa kina
zaidi namna ya kuyaendeleza kwa kuipatia nchi wataalamu wa elimu ya kati katika
michezo iwe kwa ajili ya ofisi za umma, vyuo vya elimu ya juu au ajira binafsi.
Uongozi wa sasa mnajukumu la kubadilisha mambo twende mwelekeo huo mpya,"
alisema.
Aidha, Dkt.
Abbasi amekitaka Chuo hicho pia kuanza kufikiria kuwa na mkondo wa kukuza
vipaji vya vijana wenye uwezo katika michezo kama soka wakianzia na mpira wa
kikapu na riadha kwa kuwaweka na kuwalea chini ya wataalamu na vifaa
walivyonavyo na baadaye kuwasainisha mikataba na timu kubwa ndani na nje ya
nchi.
"Nimeshangaa
kuona hapa mna makocha wa soka, kikapu, riadha, vifaa mbalimbali ikiwemo
viwanja n.k na pia mna wataalamu wa elimu ya viungo na mazoezi lakini mnaishia
kuzalisha maafisa michezo tu wa kwenda kukaa maofisini; fikirieni pia kuanza
kuzalisha wachezaji kwa kuwalea wenye vipaji kutoka nchi nzima ili baadaye
wakatumikie taifa kwenye michezo wakiwa weledi," alisisitiza.
Katika ziara
hiyo Dkt. Abbasi aliambatana na maafisa kutoka Taasisi ya Mchezaji wa Tanzania
aliyeko Aston Villa ya Uingereza, Mbwana Samatta, iitwayo Samatta Foundation,
ambao walikwenda kujionea uwekezaji uliofanywa na Serikali katika chuo hicho
kwa ajili ya kufanyakazi kwa pamoja siku za usoni.
Leo Dkt
Abbasi atatembelea miradi mbalimbali ya Serikali jijini Mwanza ikiwemo kukagua
utayari wa viwanja vya michezo kufuatia agizo la Rais Magufuli la kuruhusu
michezo kurejea chini ya tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Covid-19.
Post A Comment: