Home
Kitaifa
WAZIRI HASUNGA ATANGAZA MAZAO YATAKAYOUZWA KWENYE MFUMO WA STAKABADHI GHALANI.
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Serikali
imetangaza rasmi mazao ya kuanzia yatakayouzwa kupitia mfumo maalumu wa uuzaji
wa mazao wa Stakabadhi ghalani.
Mazao hayo
ni pamoja na zao la Korosho ambalo limekuwa na mafanikio makubwa kupitia mfumo
huo, mazao mengine ni Ufuta ambao utauzwa kwa mfumo huo katika baadhi ya maeneo
nchini.
Waziri wa
Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ametangaza msimamo huo wa serikali wakati
akizingumza ofisini kwake Jijini Dodoma juzi tarehe 30 Mei 2020 huku akiyataja
mazao mengine yaliyoingizwa katika mfumo huo kuwa ni pamoja na Choroko, Pamba,
Dengu n.k pamoja na Kahawa itakayotumia mfumo huo kwa baadhi ya maeneo.
Waziri
Hasunga amesema kuwa mfumo huo tangu umeanza kutekelezwa umekuwa na faida kubwa
hususani katika mikoa ya kusini kupitia zao la korosho lakini umeleta
changamoto kubwa katika maeneo ambayo misingi ya kuanzishwa kwa mfumo huo
haijatimizwa.
Amesema
kuwa ili mfumo wa Stakabadhi ghalani uweze kufanya kazi kwa weledi na ufanisi
mkubwa ni lazima kuwa na vyama vya Ushirika vya mazao vilivyoanzishwa na wananchi
wenyewe katika eneo husika.
Ameeleza
kuwa lengo la kuwa na vyama hivyo ni kufanya kazi ya kukusanya mazao na
kuyapeleka kwenye ghala kuu ambalo limesajiliwa na kuwa na viwango
vinavyotakiwa.
Jambo
jingine ni lazima kuwepo na muendesha ghala mwenye leseni anayetambuliwa na
Bodi ya Maghala na lazima elimu ya kutosha itolewe kwa wananchi ya namna ya
kutumia mfumo huo na ushiriki wao katika kufuatilia minada itakavyokwenda.
Amesisitiza
kuwa ili mfumo huo uweze kufanya kazi vizuri wanunuzi lazima wawepo, Mfumo
utangazwe na kuuzwa hadharani kadhalika kuwe na mzigo wa kutosha pamoja na
ubora wa uhifadhi ili kuwavutia wanunuzi.
Ameeleza
kuwa sio mazao yote yanaweza kutumika katika mfumo wa stakabadhi ghalani ni
baadhi ya mazao kulingana na uwezo wake wa kutunzwa na kukaa muda mrefu bila
kuharibika. Hivyo kwa mazao ya mboga na matunda haiwezi kuwa jambo jepesi
kuzitunza muda mrefu hivyo sio rahisi kuingia katika mfumo wa stakabadhi
ghalani.
“Ukichukua
mazao kama karanga ukaweka kwenye mfumo huu, unaweza ukahifadhi lakini tatizo
la karanga zinaweza zisiwe na unyevu unaokubalika hivyo kuna hatari ya
kusababisha Sumu kuvu.
Waziri
Hasunga amesema kuwa lengo la kuanzishwa kwa mfumo wa Stakabadhi ghalani
ilikuwa ni kulinda maslahi ya wakulima kwani mazao hukusanywa pamoja, kuwekwa
kwenye madaraja kisha kupanga bei kwa pamoja hivyo kuuza kwa bei nzuri.
Mfumo huo
unamuwezesha mkulima kupata mkopo popote baada ya kuwa na risiti ya stakabadhi
ghalani wakati akisubiri mazao yake kuuzwa kwa bei nzuri
Kwa
utaratibu mfumo wa stakabadhi ghalani unasimamamiwa na Bodi ya Maghala ambayo
ipo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara hivyo kuikabili changamoto hiyo
serikali imeihamishia Bodi hiyo wizara ya kilimo ili kupunguza muingiliano
uliopo wa kimajukumu katika Wizara hizo mbili.
Mhe Hasunga
amesema kuwa katika mikoa ambayo tayari vyama vya Ushirika vimeanzishwa mfumo
huo unafanya vizuri lakini kwa mikoa ya Dodoma, Singida, Manyara, Katavi ambapo
vyama vya Ushirika havijaanzishwa mfumo huo hauwezi kufanya kazi.
Waziri wa
Kilimo Japhet Hasunga (Mb) ametoa maelekezo kwa wakuu wa mikoa na wilaya katika
maeneo ambayo hakuna vyama vya Ushirika vilivyoanzishwa na wananchi wenyewe,
Hakuna maghala yaliyosajiliwa, na Hakuna wenye leseni wanaotambulika na Bodi ya
Maghala kutowasumbua wananchi badala yake wauze kwa uhuru katika maeneo
watakayo.
Kadhika,
Waziri Hasunga amewataka wafanyabiashara watakaonunua mazao hayo kwa mzigo
unaozidi Tani moja ni lazima Kodi za Halmashauri zilipwe kwa mujibu wa
utaratibu wa kikanuni na kisheria.
Ameongeza
kuwa moja ya majukumu ya wakuu wa Mikoa na Wilaya katika mfumo wa mazao ya
Stakabadhi ghalani ni kusimamia biashara kwa kuzingatia taratibu bila wananchi
kudhulumiwa ambapo wasimamizi ni vyama vya Ushirika, pamoja na Bodi ya Maghala.
Back To Top
Post A Comment: