ImageMAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imetoa siku saba kwa upande wa Jamhuri kuwasilisha majibu ya kiapo kinzani na maombi ya wadhamini Ibrahim Ahmed na Robart Katula wa mbunge wa zamani wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, Julai 14, mwaka huu.
Wadhamini hao amefungua maombi wakiiomba itoe hati ya kumkamata kwa kuwa wameshindwa kumpata na kumfikisha mahakamani hapo.

Maombi hayo yalipangwa kusikilizwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, lakini upande wa Jamhuri haujawasilisha majibu ya kiapo kinzani.

Hakimu Simba alisema mahakama yake itasikiliza maombi hayo Julai 14, mwaka huu na kesi ya msingi itatajwa siku hiyo.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, alidai kuwa kesi hiyo imepangwa kwa ajili ya kutajwa na kwamba amri za awali kuhusu mshtakiwa Lissu zinaendelea.

Mbali na Lissu washtakiwa wengine ni Wahariri Simon Mkina, Jabir Idrisa na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehbooh.

Katika kesi ya msingi kwa pamoja washtakiwa hao, wanakabiliwa na mashtaka matano ikiwamo kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.

Ilidaiwa kuwa kati ya Januari 12 hadi 14, 2016, jijini Dar es Salaam, washtakiwa Jabir, Mkina na Lissu, waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar.’

Katika shtaka la pili wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016 walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.

Mshtakiwa Mehboob anadaiwa kuwa Januari 13, 2016 katika jengo la Jamana lililopo Manispaa ya Ilala, alichapisha gazeti la Mawio lililokuwa na taarifa za uchochezi.

Ilidaiwa kuwa mshtakiwa huyo pia alichapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati ya sheria ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.


Share To:

Post A Comment: