Na John
Walter-Manyara
Ikiwa ni
wiki mbili tu kupita tangu Maafisa wawili wa Mamlaka ya Mapato mkoani Manyara
kukamatwa na TAKUKURU kwa tuhuma za kuomba na kupokea Rushwa ya shilingi Milioni
kumi kwa mfanyabiashara wilayani Mbulu, wengine watatu wamekamatwa kwa makosa
kama hayo.
Mkuu wa Taasisi
ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Manyara Holle Mkungu
amesema kwa sasa wanawashikilia maafisa watatu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) Mkoani hapo kwa tuhuma za kuomba na kupokea Rushwa ya shilingi Milioni
moja kutoka wa mfanyabiashara wilayani Babati.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo June 12,2020, Makungu
amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Jackline Leonard Manjira, Eva Joseph Mtandika na
Ephrahim John Medard ambao waliomba rushwa hiyo kutoka kwa mfanyabiashara wa
duka la reja reja ili wasimuongezee makadirio ya kodi katika biashara yake.
Uchunguzi wa
TAKUKURU umebaini kwamba mfanyabiashara huyo alikadiriwa kulipa kodi ya
shilingi laki mbili na nusu kwa mwaka na mtumishi wa TRA ambaye hakumdai
rushwa.
Makungu
amesema mfanyabiashara huyo akaomba kulipa kodi hiyo kwa awamu na akakubaliwa
ambapo mpaka mwezi Juni 2020, tayari alikuwa ameshalipa awamu ya kwanza ya kodi
aliyokuwa amekadiriwa.
Ameeleza kuwa
wakati akiendelea na biashara yake huku akisubiri kulipa awamu ya
pili,alifuatwa tena na watuhumiwa ambao ni Maafisa wa Mamlaka ya Mapato na
kuelezwa kuwa amekadiriwa chini ya kiwango na kwamba kwa biashara yake
alitakiwa kuwa na EFD Mashine na hivyo ametenda kosa.
Ameendelea kueleza
kuwa baada ya maelezo hayo walimtaka aende ofisi za TRA zilizopo mjini Babati
kwa hatua zaidi ambapo aliitikia wito huo na alipofika ofisini hapo akaelezwa
kuwa alikadiriwa chini ya kiwango hivyo anatakiwa kulipa kodi ya shilingi laki
nne na nusu kwa mwaka na faini ya shilingi milioni tatu kwa kutotumia mashine
ya EFD.
Makungu
amewaambia waandishi wa habari kuwa, mfanyabiashara huyo aliwaeleza maafisa hao
kuwa hawezi kulipa fedha hizo kutokana na biashara aliyonayo vinginevyo ni bora
afunge tu biashara hiyo, ambapo baada ya kutoa uamuzi huo ndipo alipofahamishwa
na afisa Jackline Manjira wa TRA Babati
ili asipigwe faini hiyo awapelekee
shilingi milioni moja.
Mkuu wa
TAKUKURU ameeleza kuwa kutokana na mwamko walionao wananchi wa Manyara kwa
sasa,mfanyabiashara huyo aliamua kutoa taarifa TAKUKURU na mtego wa shilingi
Milioni moja uliandaliwa ambao uliwezesha kukamatwa kwa watumishi hao.
Amesema uchunguzi
zaidi unaonyesha kuwa baada ya watumishi hao kukabidhiwa fedha za mtego wa
hongo,Jackline Manjira na Eva Mtandika waliandika kwenye faili la
mfanyabiashara huyo kuonyesha kuwa amesamehewa ongezeko la kodi na uamuzi wa
mashine ya EFD hadi mwaka 2021.
Watuhumiwa
hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote mara uchunguzi
utakapokamilika huku akitoa wito kwa wakazi wa Manyara na watumishi wa Umma
kuwa uadilifu sio karama au kipaji ni uamuzi wa mtu.
Post A Comment: