Na John Walter-Manyara
Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani Simanjiro mkoani Manyara kwa
kushirikiana na jeshi la polisi wilayani humo, imemfikisha katika Mahakama ya
Wilaya ya Simanjiro Afisa Mtendaji wa kata ya Langai Anna John
Mlomi kwa makosa ya kudai na kupokea rushwa ya shilingi 100,000.
Taarifa iliyotolewa leo ijumaa juni 19,2020 na mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Manyara Holle
Makungu imeeleza kuwa, kosa hilo ni
kinyume na kifungu cha 15 cha sheria ya
kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007.
Makungu
amesema mwingine aliyeunganishwa katika mashtaka hayo ni afisa mtendaji wa
kijiji cha Langai Masiar Sambana ambao walifikishwa mahakamani hapo na
mwendesha mashtaka wa jeshi la polisi Magira Marwa na kufunguliwa kesi ya jinai
namba CC 50 ya mwaka 2020.
Amesema
baada ya kusomewa makosa yao mbele ya hakimu wa mahakama hiyo Onesmo Nicodemo,
watendaji wote wawili walikana kupokea rushwa hiyo.
Taarifa ya
mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Manyara imeeleza kuwa hadi wanaondoka mahakamani hapo
,washtakiwa walikuwa hawajatimiza masharti ya dhamana yaliyowekwa na mahakama.
Aidha uchunguzi
wa TAKUKURU kuhusu shauri hilo umekamilika na kesi hiyo itatajwa tena
mahakamani hapo Julai 1,2020.
Makungu ametoa rai kwa watumishi wa Umma mkoani Manyara
na Tanzania kwa ujumla, kwamba ili kujiepusha na mkono wa sheria, wafanye rejea
kwenye maandiko ya vitabu vitakatifu
ikiwemo Quran na Biblia ambapo
katika kitabu cha biblia Luka 3:12-14, watumishi wanaohusika na ukusanyaji wa
maduhuli ya serikali waliagizwa kutotoza kuliko walivyoamriwa na kwa watumishi
wote wakatakiwa kutosheka na mishahara yao. Kwa wale wanaokaidi yaliyoandikwa katika vitabu
vitakatifu wafahamu kuwa mamlaka ziliwekwa na Mungu, hivyo wataendelea
kupambana na mkono wa sheria.
Post A Comment: