WAZIRI MKUU,
Kassim Majaliwa leo Juni 17, 2020 ametia saini kitabu cha maombolezo ya kifo
cha aliyekuwa Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza na kutoa pole kwa wananchi wa
nchi hiyo kwa niaba ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
“Kwa niaba
ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli nimekuja hapa kutoa pole na salamu
za rambirambi kwa Serikali na wananchi wa Burundi kufuatia kifo cha aliyekuwa
rais wa nchi ya Burundi. Mheshimiwa Rais na Watanzania wote tumepokea kwa
mshituko na masikitiko makubwa taarifa za kifo chake.”
Waziri Mkuu
ameyasema hayo leo (Jumatano, Juni 17, 2020) akiwa katika Ofisi za Ubalozi wa
Burundi, Upanga jijini Dar es Salaam baada ya kusaini kitabu cha maombolezo ya
kifo cha aliyekuwa Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza aliyefariki Juni 9, 2020
kutokana na mshituko wa moyo.
Amesema
Tanzania na Burundi ni nchi zenye historia ndefu na mshikamano wa muda mrefu,
hivyo ametumia fursa hiyo kuwasihi wananchi wa Burundi wawe watulivu katika
kipindi hiki cha majonzi. “Serikali ya Tanzania itaendelea kudumisha umoja na
mshikamano kati yake na Burundi.”
Awali,
Balozi wa Burundi nchini Tanzania, Balozi Abayeho Gervais ametumia fursa hiyo
kumshukuru Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa ushirikiano mkubwa
anaoutoa kwa Taifa hilo na kwamba anatarajia umoja na mshikano huo utadumu
milele na milele.
“Tunamshukuru
Rais wa Tanzania amepeleka ujumbe mkubwa Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete nchini Burundi kwa
ajili ya kushuhudia uapishwaji wa Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye ambaye
anatarajiwa kuapishwa kesho Juni 18.
Akizungumzia
kuhusu kifo cha aliyekuwa rais wa nchi hiyo Balozi Gervais amesema wamepokea
kwa mshtuko mkubwa kwa sababu alikuwa bado ni kijana akiendelea kufanya
shughuli zake. “Hii yote ni mipango ya Mwenyezi Mungu na sote tupo safarini.”
IMETOLEWA
NA:
OFISI YA
WAZIRI MKUU,
JUMATANO,
JUNI 17, 2020.
Post A Comment: