Jeshi la polisi Mkoa wa Arusha,limejipanga kutoa ushirikiano kwa waongoza utalii mkoani hapa katika kipindi hiki ambacho wanatarajia kuanza kupokea watalii kwa vingi baada ya ugonjwa wa Corona kupungua kwa kiasi kikubwa hapa nchini.
Akiongea wakati akifungua mafunzo ya siku sita ya wadau wa utalii yaliyoandaliwa na chama cha waongoza utalii Tanzania (TSG)jijini hapa,Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha,Jonathan Shanna alisema kuwa jeshi hilo lipo imara kuimarisha ulinzi katika msimu wa utalii na kuwahakikishia watalii usalama wa kutosha.
"Tutaimarisha ulinzi kila kona hakuna hata mtalii hata mmoja atakayeibiwa tunawaomba ushirikiano wenu ili kuiletea sifa nchi yetu" Alisema Shanna.
Aidha alimpongeza Rais John Magufuli kwa uongozi wake ambao umesaidia sana kupunguza maambukizo ya ugonjwa wa Corona kutokana na kuhimiza maombi ya kufukuza Corona na dawa za kujifukiza ,hivyo kutoa fursa kwa wageni kuingia nchini kwa shughuli za utalii.
Awali mwenyekiti wa TSG,Samweli Mbaga alisema wameamua kufungua mafunzo hayo kwa waongoza utalii kama njia mojawapo ya kujiweka tayari katika kupokea watalii kipindi hiki cha ugonjwa wa Corona wanaotarajia kuanza kuingia hapa nchini.
"Wakati ugonjwa wa Corona unaelekea kumalizika tumeamua kuanzisha mafunzo haya ya siku sita ili kuwajengea uwezo waongoza utalii namna ya kujikinga na kuwakinga na maambukizo ya Corona watalii." Alisema Mbaga
Alisema chama cha waongoza utalii nchini kina wanachama zaidi ya 300 hivyo wameona ipo haja ya kutoa mafunzo kwa wanachama wao ili yaendane na misingi ya wizara ya afya katika kukabiliana na ugonjwa wa Corona.
Naye Katibu wa TSG ,James Mazigo alisema changomoto inayowakumba waongoza utalii nchini ni kukosa taarifa sahihi za mwongozo wa kutangaza utalii,elimu ya utafiti wa wanyama pori na huduma ya Kwanza kwa watalii pindi kunapotokea ajali.
"Naimani katika semina hii itasaidia sana vijana kuwa na uelewa mpana wa masuala ya kuongoza utalii na tunafikiria kuendelea kutoa mafunzo haya kila Mara*Alisema Mazigo
Post A Comment: