Hayo yanasemwa
na Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya
Longido, Dkt. Jumaa Mhina wakati akizungumza na Afisa Habari kutoka Idara ya
Habari – MAELEZO na mwandishi wa makala hii, Immaculate Makilika alipokuwa ziarani huko mkoani Arusha hivi
karibuni.
Dkt. Mhina
anaendelea kusema kuwa maji yanapofika Longido kutoka Mlima Kilimanjaro
yanahifadhiwa kwenye tanki kubwa na kusambazwa ndani ya mji wa Longido kwenye
mtandao wa Km 44.7 kisha yanaenda katika Kata ya Engikaret umbali wa km 31kwa
hiyo huu ni mradi mkubwa kuwahi kutokea na wa kihistoria.
“Hivi sasa
tunavyozungumza, wananchi wanachota maji
ya bomba kwenye nyumba zao, hiyo
ilikuwa miujiza hakuna mtu ambaye aliamini kuwa jambo hili linaweza kutokea,
lakini jambo hili limetokea”, anasisiza Dkt. Mhina.
Ni dhahiri
kuwa mradi ulilenga kuongeza kiwango cha
upatikanaji wa maji katika Mji wa Longido kutoka asilimia 15 ambayo ni sawa na
wakazi 2,510 hadi kufikia asilimia 100 sawa
na wakazi 16,712 kwa sasa. Kiasi hicho cha maji kimetosheleza mahitaji kwa
asilimia 100 hadi kufikia idadi ya wakazi 26,145 kwa mwaka 2024.
Bi.Winnie
Sangau mkazi wa Longido, anasema hapo awali kulikuwa na changamoto kubwa ya
upatikanaji wa maji, kwani iliwalazimu kwenda kuchota maji sehemu yenye umbali
mrefu ambapo ni kwenye kituo kikubwa kilichokuwa kikitoa huduma ya maji mara
moja tu kwa wiki tena ambayo hukatika saa nane alasiri, baada ya mradi wa mto
Simba kuanza kutoa huduma ya maji hali hiyo imebaki historia ambayo hawatakaa
kuisahau maishani mwao kwani yalikuwa mateso makubwa kwa akina mama ambao ndio
walionekana na ndoo za maji kila uchao wakihaha kutafuta maji kama swala
aliyenusurika kujeruhiwa na nyoka mkubwa!
“Ahaa! hivi
sasa upatikanaji wa huduma ya maji ni rahisi, tunapata maji kwenye nyumba zetu
na ambao hawajavuta mabomba katika nyumba zao wanachota kwenye vituo vilivyopo
karibu na makazi ya watu na maji yanatoka kila siku, kwa kweli tunamshukuru
sana Rais Magufuli kwani amebadilisha maisha yetu wakazi wa Longido”, anaongeza
Sangau.
Mradi huu wenye uwezo wa kuzalisha maji kiasi cha mita za ujazo
2,160 kwa siku wakati mahitaji ni mita za ujazo 1,462, umefungua fursa mpya za
biashara katika wilaya hiyo muhimu ya
Longido ambapo kwa
upande wa kaskazini inapakana na nchi jirani ya Kenya, na hivyo suala la maji
ni nyenzo muhimu kwa matumizi mbalimbali hasa wakati huu ambao ulimwengu unapamba
na virusi vya Corona vinavyosababisha homa kali ya mapafu huku wengine wakisema
hii ni “vita ya tatu ya dunia”.
Akielezea
namna ambavyo mradi huo wa maji ya mto Simba umebadilisha maisha ya
wanalongido, mwalimu mstaafu, Bw.Charles Msangi anasema “Kwa sasa maji yanapatikana wakati wote usipohitaji unafunga, na hivyo sipati
shida ya huduma ya maji hapa kwenye biashara yangu ya nyumba ya kulala wageni,
namshukuru sana Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa kutukubalia huu mradi
amefanya kitu kikubwa sana ambacho watu wa Longido hatutasahau. Wafugaji huko
nyuma walipata shida sana kwani walikuwa wakienda kunywesha mifugo siku nzima
na mara nyingine ng’ombe hulala huko huko , lakini kwa sasa hawaendi tena huko kwani watu wengi wana
mabomba katika nyumba zao na sehemu za kunyweshea zimewekwa karibu na makazi ya watu”.
Halikadhalika miujiza ya Longido haikuishia kwenye maji tu, bali hata
kwenye mifugo na ukusanyaji wa mapato, hali iliyobadilisha maisha ya wakazi
wengi ambao ni wa jamii ya kimasai.
Awamu ya kwanza
ya mradi wa ujenzi wa mnada wa mifugo ulipata fedha za utekelezaji kupitia
ufadhali wa programu ya kuendeleza Miundombinu ya Masoko, Ongezeko
la Thamani na Huduma za Fedha Vijijini (MIVARF) kwa asilimia 95 na Halmashauri ya
Wilaya ya Longido ilichangia asilimia 5 ya gharama za mradi kwa awamu ya
kwanza.
Utekelezaji
wa ujenzi wa miundombinu ya mnada wa
mifugo ulianza rasmi Novemba 2016 na
kugharimu shilingi 782,743,085.59/= ambapo MIVARF imechangia 95% sawa na
shilingi 743,605,931.30 na Halmashauri ilichangia asilimia 5 sawa na shilingi 39,137,154.30.
Katika awamu ya pili ya ujenzi wa miundombinu ya mnada huu,
Wizara ya Mifugo na Kazi hii ilitoa jumla ya shilingi 150,000,000/= ili
kukamilisha ujenzi wake kazi. Hivyo jumla kuu ya gharama za mradi (awamu ya
kwanza na awamu ya pili) ni shilingi 932,743,085.59.
Licha ya mradi huo kuwa na manufaa mbalimbali kama vile kuongeza uzalishaji wa mifugo na
mazao ya mifugo kutokana na uwepo wa soko la uhakika la mifugo, kuboresha na kuinua kipato cha wananchi wa Wilaya
ya Longido kwa kuuza mifugo ndani ya Tanzania na nchi jirani.
Faida nyingine
ni ajira kwa vijana na wanawake, kurahisisha upatikanaji wa mifugo kwa ajili ya
kiwanda cha nyama kinachojengwa upande wa pili wa eneo la mnada ambacho
kitasindika mbuzi au kondoo 2,000 na ng’ombe 500 kwa siku, ikiwa ni pamoja na
na kijiji cha Eworendeke kunufaika na mapato asilimia 10 kutoka eneo la mradi.
Dkt. Mhina anasema kuwa kwa mara ya kwanza katika nchi hii, Serikali
imepata mapato makubwa kupitia mnada wa kuuza mifugo kwenda nchi jirani ya
Kenya.
“Katika mnada huo tuna mifugo takribani 3,000 hadi 6,000 kulingana na
msimu inavuka kwenda nchi ya Kenya, na mifugo hiyo imekuwa ikivuka bila
Serikali kupata ushuru wa aina yoyote yaani export
permit kwa miaka yote, lakini tulivyoanzisha mnada huu kwa kipindi cha
mwaka huu pekee tayari Serikali
imekusanya shilingi bilioni 1.2, na hivyo kiasi ambacho halmashauri inapata kwa
mwaka kutokana na mnada huu ni shilingi milioni 400 na hivyo kuongeza mapato ya
halmashauri ambapo inatusaidia kupeleka fedha katika miradi ya maendeleo pamoja
na kulipa stahili“ anasema Dkt. Mhina.
Dkt. Mhina anaendelea kusema kuwa ili kuongeza mnyororo wa thamani licha
ya kuwa na soko la kimataifa la mifugo, wilaya yake tayari imepata muwekezaji anayejenga
kiwanda kikubwa kuchakata nyama katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati
ambacho ambacho ujenzi wake utakamilika mwezi Julai mwaka huu.
Aidha, anaongeza, “Tunaamini kuwa kiwanda hicho kitakapoanza kufanya
kazi, kitakuza uchumi wa wilaya yetu, na
watu watafuga kwa tija, tumeshaongea na benki mbalimbali pamoja na vikundi
zaidi ya 100 vya wafugaji na
wafanyabiashara wa mifugo na hivi sasa tumeanzisha SACCOS ya kununua na kuuza
mifugo ili kiwanda kitakapoanza kazi watanzania wasibaki kuwa watazamaji“
Mmoja wa wawekezaji wa kiwanda hicho cha Eliya Food
Overseas Ltd, Alshabir Mohamed anasema kuwa gharama za mradi huu ni jumla
ya Dola za Kimarekani 5,000,000.
Ujenzi wa kiwanda hicho umefikia asilimia 80, na wanatarajia kiwanda
hicho kuanza kazi ifikapo mwezi Julai mwaka huu, ambapo watapeleka nyama yao
kwenye hoteli mbalimbali za hapa nchini pamoja na kusafirisha nje ya nchi.
“Kiwanda hiki kitatumia kila kitu kinachotoka kwa mnyama ili kutengeneza
malighafi mbalimbali, ngozi zote zitapelekwa katika kiwanda cha ngozi
Mororgoro, pia tutatengeneza chakula cha mifugo, mafuta yanayotoka kwenye
wanyama yatatumika kutengeneza sabuni. Aidha, tutaajiri watu 3,000 ambao wengi
wao watakuwa vijana“, anasema Mohamed.
Hakika mapinduzi yanayoendelea katika Wilaya ya Longido, ni dhahiri kuwa
Serikali imedhamiria kuboresha maisha ya watanzania na kufikia azma yake ya
nchi ya uchumi wa kati ifikapo 2025,
sambamba na Tanzania ya viwanda.
Post A Comment: