Na John Walter-Manyara
Klabu ya
wapinga Rushwa katika chuo cha ufundi stadi (VETA) Mkoa wa Manyara imesema
katika kipindi cha mwaka 2020, imejipanga kuhakikisha vitendo vya rushwa
vinatokomezwa kwa vitendo.
Hayo yameelezwa
na mwenyekiti wa Klabu ya wapinga Rushwa katika chuo cha ufundi Stadi Manyara (VETA) Juma Manyanya wakati wa hafla fupi ya
kuwakaribisha wanachama wapya katika klabu hiyo iliyofanyika chuoni hapo.
Amesema katika kufanikisha hilo wameandaa mpango wa kutoa elimu ya umuhimu wa kupinga rushwa kwa
wanafunzi wenzao, kila siku asubuhi wakiwa wamekusanyika kabla ya kuingia darasani hutoa elimu hiyo kwa ufupi.
Manyanya ameeleza
kuwa wanao mpango wa kufanya ziara za
midahalo juu ya kupinga rushwa katika shule na vyuo jirani wilayani Babati.
Pamoja na
hayo amesema Klabu ya wapinga rushwa VETA Manyara, imeandaa bustani ya miti mbalimbali ya kuuza,kuwa na mfuko wa
tawi la Klabu rushwa Veta Manyara pamoja na kuwa na sare (Fulana) kwa kila mwanachama.
Mwenyekiti huyo amempongeza Rais John Magufuli na
serikali yake kwa namna alivyopambana na rushwa huku akiahidi kuwa wataendelea
kuhamasishana katika vita hivyo.
Kwa upande
wa mkuu wa Dawati la Elimu kwa Umma kutoka Taasisi ya kuzuia na kupambana na
Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Manyara Sultan Ng’aladizi amesema Pamoja na mafanikio
ya TAKUKURU huo yanayotokana na elimu
waliyoitoa kwa jamii juu ya mapambano hayo,Taasisi hiyo pia imeendelea kuvitembelea
vilabu vya kupinga Rushwa katika shule
na Vyuo ili kuwajengea uwezo.
Amesema rushwa inaweza kuzuia nchi isifike
kwenye uchumi wa kati wa viwanda kama nguvu ya pamoja na ushirikiano
hautakuwepo kuikabili, hivyo kwa
kushirikisha wanafunzi wa vyuo mbalimbali hapa nchini itasaidia kwa kiwango
kikubwa suala la rushwa kupotea katika jamii.
Alisema vita
dhidi ya rushwa ni tatizo la jamii na dunia hivyo Serikali pekee pamoja na
mafanikio iliyoyapata, haiwezi kuimaliza bila kushirikisha wanafunzi katika ngazi
zote za msingi hadi vyuoni.
Amewatia
moyo wanafunzi hao kwa kuwaeleza kuwa katika vita dhidi ya rushwa kuna vikwazo
vingi lakini ni Lazima wapambane kuanzia
sasa ili kuikabili.
Amewaeleza
kuwa “kila jambo linawezekana, hivyo rushwa kumalizika inawezekana lakini mapambano bado yanahitajika kwa nguvu kubwa ya pamoja ili kuhakikisha inatokomezwa”.
Amesema Maadili
sio karama kwamba mtu anatunukiwa bali ni mtu mwenyewe kuamua.
Alisema Rushwa ni adui aliyejiwekea mizizi
anayeendelea kuathiri maisha ya mwanadamu na hufanyika kwa siri ndio maana ni
ngumu kumkabili, rushwa inasababisha wananchi kukosa imani na serikali yao,
inaongeza matabaka ambapo walio masikini huumia zaidi hivyo wanafunzi wakiwa na
uelewa itarahisisha kumuondoa adui huyo.
Post A Comment: