HATIMAYE
Kiwanda cha kwanza kikubwa chenye uwezo wa kutakasa dhahabu na madini mengine
kwa ubora wa mahitaji ya soko la kimataifa sasa kimeanza rasmi uzalishaji
nchini.
Kiwanda
hicho kinachojulikana kama Eyes of Africa Ltd ( EOA) kimeanza uzalishaji wake
kwa uwezo wa kutakasa dhahabu na madini mengine kwa kati ya kilo 30 hadi 50 kwa
siku, huku shabaha iliyopo ni kufikia kilo 1000 ifikapo 2021.
Waziri wa
Madini Doto Biteko, mnamo Agosti 20 mwaka jana wakati akikagua maendeleo ya
ujenzi wa kiwanda hicho alisisitiza mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wake
kitatoa fursa kwa Wafanyabiashara nchini kusafisha dhahabu zao, lakini
kitawezesha Taifa kuwa na akiba ya madini yenye ubora wa viwango vya kimataifa
kufikia asilimia kupitia Benki Kuu ya
Tanzania
Aidha,
Januari mwaka jana, Rais John Magufuli aliagiza BoT kuwa na akiba ya dhahabu na
kuhimiza haja ya Serikali kudhibiti usafirishaji wa madini kutoka hapa nchini.
Ambapo Tanzania ni nchi ya 4 kwa kuzalisha dhahabu ikitanguliwa na Afrika
Kusini, Ghana na Mali.
Biteko
alisema mara baada ya kukamilika kwa kiwanda hicho BoT itaanza kununua dhahabu
iliyotakaswa ambayo itawekwa kwenye akiba ya Taifa ya dhahabu na hatimaye
kusaidia taifa kuanza kuuza dhahabu yenye ubora kiushindani kwenye soko la
kimataifa.
"Hatua
ya Serikali kutoa leseni ya kuanzisha viwanda vya namna hii ni takwa la
kisheria kutokana na mabadiliko ya hivi karibuni ya sheria ya madini."
alisema Biteko.
Akizungumza
na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya kiwanda hicho, kilichopo pembezoni
mwa Kiwanja cha Ndege jijini Dodoma mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi Mkuu wa EOA,
Ferenc Molnar alisema kwa sasa ujenzi umekamilika kwa asilimia 100, mitambo
yote imekwishafungwa na uzalishaji umeanza.
Molnar
alisema kupitia kiwanda hicho Taifa linakwenda kuongeza thamani ya dhahabu na
madini yake mengine kutoka kati ya asilimia 70 na 90 iliyopo kwa sasa na
kufikia kiwango cha asilimia 99.99 kinacho kubalika kwenye soko la kimataifa.
Mkurugenzi
huyo mkuu mbali ya kuwakaribisha wafanyabiashara wote na taasisi nyingine
zilizo kwenye mnyororo wa uzalishaji wa madini, aliweka bayana kwamba kwa sasa
wapo mbioni kusaini mkataba wa utendaji wa pamoja na Shirikisho la Wachimbaji
Wadogo wa Madini (FEMATA).
"
Tutaingia mkataba na FEMATA kwa sababu fedha inayotokana na mauzo ya dhahabu
yao huwa moja kwa moja inarudi nchini na kunufaisha Taifa kwa ujumla...lakini
wachimbaji wakubwa wanapochimba dhahabu huisafirisha nje ya nchi na huishia
huko huko labda sana watalipa mrahaba pekee." alisema Molnar.
Alisema
sababu nyingine ya kufanya kazi na wachimbaji wadogo ni kuwawezesha kuanza
kukopesheka kwenye taasisi za fedha na zaidi kuimiliki na hatimaye kupata
thamani halisi kupitia mauzo ya dhahabu iliyotakaswa.
Molnar
alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi wazalishaji wakubwa wa dhahabu ambapo
uzalishaji wake kwa sasa unafikia kati ya tani 4.5 hadi 5 kwa mwezi, na
uzalishajj wake kwa mwaka kufikia tani 60.
"
Tunapozalisha dhahabu ambayo imetakaswa tutakuwa na soko la uhakika na
itakubalika kwenye vyombo vyote vya fedha...na Taifa litapata mapato stahiki.
Uwepo wa kiwanda hiki utampunguzia mzalishaji gharama kubwa ya kusafiri nje ya
nchi ili kupata huduma kama hii." alisema Molnar na kuongeza;
"FEMATA
na wazalishaji wengine wa madini kupitia kiwanda hiki sasa wataweza kwenda
benki na kuhifadhi dhahabu, kukopesheka na hatimaye kuruhusu iuzwe
pale tu bei ya soko la dunia itakapokuwa nzuri."
Kwa upande
wake Mtendaji Mwendeshaji wa Kiwanda cha EOA, Prince Mugisha alisema lengo la
Tanzania kwa sasa ni kuhakikisha tunapata thamani halisi kulingana na madini
yaliyopo, wachimbaji wengi kwa sasa hujikuta wakiuza dhahabu peke yake wakati
inapochimbwa inakuwa na madini mengine ambatani, ikiwemo Fedha, Platnum, Brass
na mengineyo.
Kwa mujibu
wa sheria ya madini nchini rasilimali hiyo haipaswi kuuzwa ikiwa katika hali
ghafi. Hivyo kiwanda hiki kitakuwa na uwezo wa kubaini madini mengine yaliyopo
ndani ya dhahabu, kuyatayarisha kwa maana ya kuyatakasa na kuyapeleka sokoni
katika hali ya ubora na viwango vya soko kimataifa." alisema Mugisha.
Post A Comment: