Na. Dennis Gondwe, DODOMA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma inatarajia ufaulu mzuri kwa wanafunzi watakaofanya mtihani wakumaliza kidato cha sita mwaka 2020 kufuatia wanafunzi hao kuandaliwa vizuri na kupata muda wa kufanya marudio kwa mada walizofundishwa. 

Kauli hiyo ilitolewa na afisa elimu sekondari wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwalimu Upendo Rweyemamu alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuelezea utimilifu wa maandalizi ya mtihani wa kumaliza kidato cha sita mwaka 2020 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.

Mwalimu Rweyemamu alisema kuwa maadalizi kuelekea mtihani huo yamekamilika na vifaa vimewasili katika shule husika kwa ajili ya mtihani huo.


 “Wanafunzi wameandaliwa vizuri kitaaluma na kisaikolojia. Nichukue nafasi hii kutoa wito kwa walimu wanaowafundisha wanafunzi wa bweni kuendelea kuwaandaa wanafunzi kisaikolojia. Kwa wanafunzi wa kutwa, wazazi wachukue jukumu la kuwapa ushirikiano mzuri na kuwaandaa wanafunzi hao kisaikolojia. Huu ni mtihani kama mitihani mingine” alisema Mwalimu Rweyemamu. 

Akiongelea matarajio ya ufaulu katika mtihani huo, afisa elimu sekondari huyo alisema kuwa Halmashauri hiyo inatarajia kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu. 


“Hali ya ufaulu itaongezeka kutokana na maandalizi yaliyofanyika, ukiangalia mada nyingi zilikuwa zimekamilika mapema kabla ya kuanza mapumziko ya corona. Nitumie nafasi hii kuwatakia heri wanafunzi wote katika Jiji la Dodoma watakaofanya mtihani huo na kuwaombea ufaulu mzuri” alisema Mwalimu Rweyemamu kwa kujiamini. 

Kwa upande mzazi Juliana Mdeme alisema kuwa maandalizi yamekamilika na mtoto wake amejiandaa vizuri. 


“Unajua miaka hii wazazi wanawajibu mkubwa kusimamia elimu ya Watoto wao ili kuhakikisha wanafanya vizuri katika masomo yao. Utakumbuka katika mapumziko ya mapambano ya corona tulikuwa na jukumu kubwa la kuwasimamia wanafunzi wetu kwa kuwapangia ratiba na kusimamia ratiba hizo. Matumaini yangu watafanya vizuri. Niishukuru idara ya elimu sekondari katika Jiji letu la Dodoma kwa kuweka msingi mzuri uliowasaidia wanafunzi kumaliza masomo yao mapema na kuwapa muda mrefu wa kufanya marudio” alisema Mdeme huku akionesha matumaini makubwa.  

Mtihani wa kumaliza kidato cha sita utafanyika nchini kuanzia tarehe 29 Juni, 2020 na kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma yenye vituo 12 vya mtihani wa kumaliza kidato cha sita vyenye jumla ya watahiniwa 1,321, mtihani huo utafanyika kwa muda wa wiki mbili.
Share To:

Post A Comment: