Na John
Walter-Babati
Watu watatu wamekufa katika ajali ya barabarani iliyotokea
katika kata ya Mamire wilayani Babati
mkoani Manyara.
Akitoa taarifa leo June 16.2020, Kamanda wa polisi mkoa wa
Manyara Paul Kasabago amesema, ajali hiyo iliyotokea june 13 mwaka huu, imehusisha gari lenye namba za usajili SU.417 aina ya Toyota
Land Cruiser mali ya shirika hifadhi za Taifa (TANAPA), iliyokuwa katika doria maalum katika maeneo hayo
yanayopakana na hifadhi ya Taifa ya Tarangire majira ya saa 2:45 usiku.
Kamanda wa
Polisi mkoa wa Manyara Paul Kasabago akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo,
amesema gari hilo lililokuwa linaendeshwa na dereva ambaye bado majina yake
hayajafahamika, iligonga pikipiki yenye namba za usajili MC 313 BKU aina ya
Boxer iliyokuwa ikiendeshwa na Said Ally (35) mkazi wa Mamire akiwa amewapakia
abiria wawili (mshkaki) kinyume na sheria za usalama barabarani.
Kasabago
amesema kuwa dereva wa pikipiki hiyo na abiria wote wawili aliokuwa amewabeba walipoteza
maisha papo hapo.
Aidha Kamanda
Kasabago ametaja majina ya waliopoteza maisha ni Said Ally (35), Elimina Herman
(22) na Renatha Salutali (17) wote wakazi wa kijiji cha Mamire.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Paul Kasabago,
mtuhumiwa alitoroka mara baada ya kusababisha ajali hiyo na kwamba jeshi hilo kwa kushirikiana na wananchi wanaendelea kumtafuta ili kujibu tuhuma
zinazomkabili.
Kamanda ameeleza
kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa gari hilo kushindwa kuchukua
tahadhari za usalama bara barani.
Miili ya
marehemu imefanyiwa uchunguzi wa kidaktari na kukabidhiwa ndugu kwa mazishi.
Post A Comment: