Na Mwandishi Wetu, Mwanza
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali leo ametembelea kuona maendeleo ya ujenzi wa meli mpya, chelezo na ukarabati wa meli mbili za New Victoria na MV Mwanza (zamani Butiama) na kuwahakikishia watanzania miradi yote hii itakamilika kwa wakati.
Akiwa kwenye maeneo ya ujenzi jijini Mwanza leo (tarehe 8.06.2020) Dkt. Abbasi amesema ujenzi wa meli hizo na Chelezo ni uthibitisho kuwa Serikali imetimiza wajibu wake bila kuchelewa ambapo imeshatoa zaidi ya Shilingi Bilioni ya 100 katika miradi hiyo minne kati ya TZS Bilioni 153.
"Hapa tulipo ni uthibitisho wa dhana kwamba si tu angani, wodini, relini au madarajani kazi kubwa zinafanyika lakini hata majini nako mnajionea Rais Magufuli anatekeleza maono yake na ndoto za Watanzania kila eneo," alisema na kufafanua kuwa miradi mitatu ambayo ni ujenzi wa Chelezo kubwa kuliko zote katika ukanda wa Ziwa Victoria, ukarabati wa meli ya New Victoria na ukarabati wa meli ya MV Mwanza kila kimoja kimefikia asilimia 98.
Kuhusu mradi wa nne wa uundaji wa meli mpya na ya kisasa na itakayokuwa kubwa kuliko zote zilizowahi kufanyakazi katika Ziwa Victoria itakayobeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo, Dkt Abbasi alisema ujenzi wake sasa umefikia asilimia 60.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Marine Services, Eric Hammis, alisema kuwa miradi iliyofikisha asilimia 98 kimsingi ilikuwa tayari lakini inasubiri wataalamu kutoka Korea wafikie kwa ajili ya majaribio.
"Wataalamu hao wamechelewa kuja kutokana na zuio la Corona lakini sasa tayari wamethibitisha kuwasili hapa nchini katikati ya mwezi Juni, 2020 ili kufanya majaribio na kisha kuruhusu chelezo na meli za New Victoria na MV Mwanza ziweze kuanza kazi wakati wowote mwezi huu," alisema Eric
Post A Comment: