Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Deo Ndejembi akishiriki ujenzi wa Shule ya Sekondari inayojengwa kwenye kata ya Chamkoroma wilayani Kongwa.
Msingi ambao umechimbwa na Wananchi wa Kata ya Chamkoroma kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari inayojengwa kwenye kata hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Deo Ndejembi akizungumza na wananchi wa Kata ya Chamkoroma alipofika kukagua ujenzi wa Shule ya Sekondari inayojengwa kwenye kata hiyo.
Wananchi mbalimbali wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Kongwa ,Deo Ndejembi ambaye alifika katika kata hiyo kushiriki na kukagua ujenzi wa Shule ya Sekondari inayojengwa kwenye kata hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, Deo Ndejembi hii leo ameongoza zoezi la uchimbaji msingi ujenzi wa Shule ya Sekondari katika Kata ya Chamkoroma wilayani humo ambayo ikikamilika itakua ikihudumia wanafunzi kutoka vijiji saba vya kata hiyo.
DC Ndejembi pia ameahidi kuchangia mifuko 10 ya Saruji ili kuwezesha kukamilika mapema kwa Shule hiyo ambayo itaenda kumaliza changamoto ya watoto wanaotembea umbali mrefu kwenda Shule ilipo.
Akizungumza na wananchi wa kata hiyo, DC Ndejembi amewapongeza kwa kujitoa kwa pamoja kama wazazi kusaidia ujenzi wa Shule hiyo lengo likiwa kumuunga mkono Rais Dk John Magufuli kwa maendeleo makubwa aliyoyafanya kwenye sekta ya elimu.
DC Ndejembi amewataka wananchi wa Kata hiyo kuhakikisha pia watoto wao wanaripoti shuleni Juni 29 kama ambavyo Rais alielekeza na Mzazi yoyote ambaye atakwamisha mtoto kuripoti atachukuliwa hatua.
" Niwaase wote kwa Umoja wenu kama mlivyojitokeza kwenye ujenzi wa Shule hii basi mhamasishane watoto kurejea shuleni Juni 29 baada ya likizo ndefu iliyosababishwa na Corona. Hatutomvumilia yoyote ambaye mtoto hatorejea shuleni.
Mimi binafsi nitachangia mifuko 10 ya saruji lakini niwaambie hii Shule ni yetu sote hapa nafahamu kuna wachimbaji wa Madini kwenye hii kata niwatake nao kusaidia ujenzi wa Shule hii siyo wachimbe Madini wapate hela halafu hawasaidii huduma za jamii," Amesema DC Ndejembi.
Katika hatua nyingine DC Ndejembi ametoa maagizo kwa Wakala wa Misitu (TFS) wilayani humo kuwakamata wale wote ambao wanachoma misitu na kulisha mifugo kwenye maeneo ya misitu.
" Hatuwezi kuruhusu uharibifu wa mazingira kwa sababu ya maslahi ya watu wachache. TFS hakikisheni mnakamata wote ambao wanalisha mifugo yao huku na kukata miti," Amesem DC Ndejembi.
Post A Comment: