Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tamisemi, Selemani Jafo akimkabidhi vitendea kazi Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Tarura, Florian Kabaka baada ya kuizindua bodi hiyo leo jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tamisemi, Selemani Jafo akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa Bodi ya Ushauri ya Tarura leo jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tamisemi, Selemani Jafo akizungumza na wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Tarura na watendaji wake leo jijini Dodoma.
Mtendaji Mkuu wa Tarura, Victor Seff akizungumza wakati wa uzinduzi wa bodi ya Ushauri ya Wakali wa Barabara Mjini na Vijijini (Tarura) leo jijini Dodoma.
Charles James, Michuzi TV
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais-Tamisemi, Selemani Jafo amemtaka Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (Tarura), Victor Seff kuwachukulia hatua watendaji wote wababaishaji kwenye ngazi ya Mikoa na Halmashauri.
Jafo amesema kuna watumishi katika ngazi za Mikoa ambao wamekua wakikwamisha spidi ya wakala huo katika kuwaletea maendeleo watanzania.
Waziri Jafo ametoa agizo hilo leo jijini Dodoma wakati wakati akiizindua rasmi Bodi ya Ushauri ya Tarura ambayo itakua chini ya Mwenyekiti wake, Florian Kabaka.
" Haiwezekani wakati huu ambao wananchi wanaikubali kazi kubwa inayofanywa na Tarura awepo mtu ambaye anatukwamisha, ni maelekezo yangu kwa Mtendaji mkuu kuwafyekelea mbali wale wote wanaotukwamisha," Amesema Jafo.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri Jafo ameitaka bodi hiyo kuendeleza kazi nzuri ambayo imekua ikifanywa na Tarura lakini pia akiisisitiza ubora wa kazi na kuweka uzalendo mbele.
Amesema wakala wa barabara umefanya kazi kubwa ndani ya kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa Rais Magufuli ikiwa ni pamoja na kujenga na kukarabati barabara na madaraja maeneo mengi nchini.
" Tarura imefanya kazi kubwa sana ya kurudisha imani ya wananchi wetu kwa serikali katika suala zima la uboreshaji wa miundombinu huku pia wakala huo ukilifanya Jiji la Dodoma kuongoza kwa kuwa na mtandao mkubwa wa lami ikiwa ni mafanikio makubwa ambayo yametokea ndani ya muda mfupi.
Bila kazi nzuri inayofanywa na Tarura wakulima vijijini hawawezi kusafirisha mazao yao kutoka kijijini kuja mjini, lakini hata wafugaji hawatoleta mifugo yao mjini kwa ajili ya biashara, hivyo Tarura mnapaswa kuelewa nyie ni kiungo muhimu kwenye mafanikio ya wetu," Amesema Jafo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi hiyo ya ushauri, Floriana Kabaka amemshukuru Rais Dk John Magufuli kwa kumteua kuongoza bodi hiyo ambayo ndio mara ya kwanza imeanzishwa.
" Tunamshukuru Rais kwa kumuamini ni wajibu wetu kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha Tarura inakua zaidi ya ilivyo sasa katika kuwahudumia watanzania wenzetu," Amesema Kabaka.
Post A Comment: