Na Mwandishi Maalum - Morogoro

WAZAZI na walezi wamehimizwa kuzingatia kuavaa barakoa kila wanapowapeleka watoto wao hospitalini, vituo vya afya na zahanati kupatiwa huduma mbalimbali za kiafya ikiwamo zile za chanjo.

Rai hiyo imetolewa leo Mkoani hapa na Ofisa Miradi kutoka Ofisi ya Mpango wa Taifa wa Chanjo (IVD), Dk. Furaha Kyesi alipozungumza na wazazi na walezi waliofika katika Zahanati ya Madizini iliyopo Kata ya Mtibwa Wilayani Mvomero kupata chanjo na kupima uzito wa watoto wao.

Maofisa wa Mpango huo wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wa Mkoa wa Morogoro na wa Manispaa wako katika ziara ya kukagua utoaji huduma za chanjo katika Mkoa huo kwa kushirikiana na Shirika la Engender Health kupitia Merck Sharp & Dohme B.V (MSD).

Dk. Kyesi amesema huduma za chanjo nchini hazijasitishwa bado zinaendelea kutolewa kulingana na ratiba za watoto walizopangiwa na kulingana na umri wao hata hivyo jambo la msingi ni kila mmoja kuhakikisha anajikinga kila anapompeleka mtoto.

“Kila mmoja anapaswa kuvaa barakoa, jikinge ili uwakinge na wengine kwa sababu hapa hakuna anayejua mwenzake ametoka wapi, amekutana na nani hadi amefika hapa kwenye zahanati.

“Ukiwa umevaa barakoa inasaidia kukukinga lakini pia unawakinga na wale wanaokuzunguka, vile vile mnapofika hapa kituoni zingatieni kunawa mikono na kukaa umbali wa mita moja, hakikisha unapokaa mkono wako ukiunyoosha hauwezi kugusa bega la mwenzako aliye pembeni yako,” amesisitiza Dk. Kyesi.

Amesema ni muhimu pia mama kuzingatia kunawa au kutakasa mikono kila anapohitaji kumnyonyesha mtoto wake ili aendelee kumkinga naye pia, watoto wadogo hatushauri wavalishwe barakoa.

Awali, Muuguzi wa Zahanati hiyo, Eliainenyi Tarimo amesema kila mwezi wamelenga kuwachanja watoto 34 lakini kwa kuwa jamii ina mwamko mkubwa wa chanjo wamefanikiwa kuvuka lengo hilo na kuchanja watoto zaidi ya 100.

“Tunaendelea kutoa chanjo kwa kuzingatia mwongozo tuliopewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wa kujikinga tusipate maambukizi.” Amesema Eliainenyi na kuendele kusema  kuwa kabla ya mzazi au mlezi kuingia ndani ya kituo hicho kwanza anatakiwa kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni ambapo ndoo imewekwa katika eneo la kuingilia katika Zahanati hiyo.

Eliainenyi amesema awali utaratibu waliokuwa wakiutumia kabla ya kuchukuliwa kwa tahadhari ya mlipuko wa Corona walikuwa hawana kabisa utaratibu huo.

“Walikuwa tu wakifika wanakwenda moja kwa moja sehemu ya kuweka kadi, wanakaa kwenye mabenchi na kusubiri kuitwa majina, tukaona tuanze kuwapa namba na kuwaruhusu wakae kwa kupeana nafasi ya mita moja kwenye mabenchi.

“Mabenchi tuliyonayo hayatoshelezi lakini eneo letu ni kubwa hivyo wanakaa na hapo nje kwa kupeana nafasi, tunapomaliza kumhudumia mtoto, tunawaomba waondoke mapema kwenda nyumbani na si kuendelea kukaa hapa,” amesisitiza.

Amesema changamoto pekee inayowakabili sasa ni wazazi na walezi hao kuwa na mwitikio mdogo wa uvaaji barakoa jambo ambalo hawachoki kuwasisitiza na kuwahimiza kuzingatia ili kuendelea kujikinga.

Amesema kwa upande wa chanjo ya HPV ambayo hupatiwa wasichana wenye umri wa miaka 14 iliyokuwa ikitolewa shuleni na kwa kuwa sasa zimefungwa kutokana na mlipuko wa CORONA, hivi sasa zinaendelea kutolewa katika Zahanati hiyo.

“Japo bado hatujawaona wengi wakija, wachache wameshakuja tumewachanja, tunaendelea kuwahimiza waje kupitia watoa huduma za afya wa ngazi ya jamii (CHW’s) na hapa kituoni huwa tunawaeleza wanajamii wanaokuja kliniki kwamba waende wakawahimize wasichana waje kupata chanjo ya pili,” amesema.

MWISHO
Share To:

Post A Comment: