3.JPG
Wananchi wakiingia katika Kituo cha Afya Mtego wa Simba kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa kukabiliana na Ugonjwa wa Corona kwa kunawa mikono kwa maji yanayoririka na sabuni na kukaa umbali wa zaidi ya mita moja kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine.

4.JPG
  Afisa Afya wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Lugata akitoa elimu kwa wananchi kuhusu ugonjwa wa Corona.kwa wananchi waliofika katika Kituo cha Afya Mtego wa Simba Wilaya ya Morogoro Vijijini kupata huduma za afya.  

5.JPG
Afisa Miradi kutoka Mpango wa Taifa wa Chanjo, unaosimamiwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Furaha Kyesi (kushoto) akimzungumza jambo na Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Mtego wa Simba, Luambano Ally.

1.JPG
Bi. Ipyana Mwamwala Muuguzi Mkunga wa Kituo cha Afya Mtego wa Simba akimpima uzito mtoto Niran Daudi (7) pembeni ni mama wa mtoto huyo, Bi. Joyce Mwantobe.

2.JPG
Bi. Elinivoniia Mchomvu Muunguzi Mkunga akisoma kitabu cha afya ya mtoto kabla ya kutoa chanjo katika Zahanati ya Fulwe, Wilaya ya Morogoro VIjijini.

 Mwandishi Maalum - Morogoro
Huduma ya chanjo za mkoba hasa katika maeneo ya pembezoni (vijijini) zinapaswa kuendelea kutolewa kwa watoto chini ya miaka mitano ili kuhakikisha wote wanafikiwa kwa wakati unaopaswa, licha ya kuwapo kwa janga la Corona.

Pamoja na kundi hilo, kundi jingine linalopaswa kufikiwa na kupatiwa chanjo ya ni wasichana wenye umri wa miaka 14 ambao wanapaswa kupatiwa ile ya HPV inayokinga dhidi ya maambukizi ya virusi hivyo vinavyosabisha ugonjwa wa saratani ya kizazi.

Rai hiyo imetolewa na Ofisa Miradi kutoka Mpango wa Taifa wa Chanjo wa Wizara hiyo, Dk. Furaha Kyesi alipozungumza na uongozi wa Kituo cha Afya Mtego wa Simba, kilichopo Wilaya ya Morogoro Vijijini, mkoani Morogoro wakati wa ziara ya ukaguzi wa huduma za chanjo zinazotolewa kwenye vituo vya afya kipindi hiki cha mapambano dhidi ya janga la Corona.

Timu ya ufuatiliaji huduma za chanjo kutoka Mpango wa Taifa wa Chanjo (IVD) wa Wizara hiyo, maofisa chanjo wa Mkoa wa Morogoro na wa Wilaya hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Engeder Health kupitia Merck Sharp & Dohme B.V (MSD), wapo mkoani humo kukagua namna huduma za chanjo zinavyoendelea kutolewa katika kipindi hiki cha janga la Corona.

“Kundi hili la wasichana lazima tuhakikishe tunalifikia, kwa sababu hawa awali msisitizo ulikuwa kuwapa chanjo kwa kuwafikia shuleni, lakini sasa shule zimefungwa kutokana na janga la Corona, lakini tunahitaji kuwafikia.

“Watoto chini ya miaka mitano nao lazima tuwafikie ili kwamba wakati tunapambana na Corona tuhakikishe pia tunaendelea kuwapa chanjo dhidi ya magonjwa mengine kama vile surua, polio, kuharisha na mengineyo, ili tusije tukapata mlipuko wa magonjwa,” amesema.

Kyesi ameshauri kwamba watoa huduma za afya waendelee kuzingatia mwongozo wa kujikinga na kufikia maeneo ya pembezoni hasa huko vijijini kuwapa huduma.

Awali akizungumza, Muuguzi Mkunga wa Kituo hicho, Ipyana Mwamwala alisema kila mwezi hupokea watoto wapatao saba na kuwapa chanjo mbalimbali kulingana na umri wao.

Amesema kituo hicho kimezungukwa na vijiji vinne ambavyo ni Sangasanga, New Land, Mkono wa Mara, Mkambarani na Mtego wa Simba (chenyewe).

“Wakina mama bado wana mwamko wa kuleta watoto kituoni lakini tunahitaji kwenda outreach kwa ajili ya kuwafikia pia wale ambao hawaji kituoni, vijiji vipo mbali na hapa,” amesema.

Ameongeza “Tupo tayari kwenda, tunatambua, tumetangaziwa kuna ugonjwa wa COVID -19 nchini ambao unatokana na maambukizi ya virusi vya Corona, hata hapa kituoni tumechukua hatua na hata tukienda kule tutazingatia kanuni zote za kujikinga sisi wenyewe na wale tunaokwenda kuwahudumia wasipate maambukizi.

Mganga Mfawidhi wa Kituo hicho, Luambano Ally amesema kutokana na taarifa hiyo ya tahadhari iliyotolewa na Wizara ya Afya, walilazimika kuchukua hatua za kuimarisha kujikinga ikiwamo kuweka ndoo za maji katika maeneo ya kuingia ndani ya kituo hicho.

“Kwenye milango yote ya kuingia ndani ya kituo kuna ndoo ya maji safi tiririka na sabuni lazima mtu anawe ndipo aingie huku ndani, lakini kama amejisahau kunawa pale au anahitaji tena kunawa akiwa humu ndani, kuna ndoo nyingine tumeweka ataweza kunawa pia.

“Hapa kituoni tumewapa taarifa kwamba kila anayekuja kupata huduma lazima avae barakoa, utaona hilo wanakijiji wanalitii na wamekuwa na mwamko, wanakuja wakiwa wamevaa, wananawa mikono, wanapata huduma na kurudi zao nyumbani,” amesema Ally.
Share To:

Post A Comment: