Nteghenjwa Hosseah, OR-TAMISEMI
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo ameiagiza Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Elimu Kibaha kutumia rasilimali za shirika kujiimarisha kiuchumi.
Jafo alitoa agizo hilo jana jijini hapa wakati wa kuzindua bodi mpya ya Shirika hilo inayoongozwa na Profesa Raphael Chibunda.
Alisema Shirika limekuwa na rasilimali nyingi ikiwamo ukubwa wa ardhi ambao kama bodi itafanya ubunifu itaweza kuitumia kufanya uwekezaji wenye tija utakaosaidia shirika kujiimarisha kiuchumi na kujitegemea.
Hata hivyo katika kutekeleza hilo, Jafo alionya uongozi wa shirika na bodi ya shirika hilo kuwa makini na uwekezaji ambao wataamua kuufanya na kusisitiza kuwa ni lazima kuwe na uwekezaji wenye tija ambao utakuwa na manufaa.
“Shirika la Elimu Kibaha lina ardhi kubwa sana, ambayo kama mtakuwa wabunifu mtakuja na uwekezaji ambao utasaidia sana kuimarisha uchumi wa shirika, mnaweza kuja na maduka ya kisasa pale.
“ Lakini nitoe angalizo, ni lazima uwekezaji mtakaoamua kuufanya muwe makini kwa kuwa na uwekezaji wenye tija, maana kunawatu wajanja wanaweza kuja na maandiko yao feki na kufanya uwekezaji ambao hauna tija.”
Aidha, Jafo alisema ni vyema Bodi hiyo ikaandeleza na kuchagiza maono ya Baba wa Taifa, Julius Nyerere ambaye aliamua kuanzisha Shirika hilo ili kupambana na maadui watatu ambao ni ujinga, maradhi na umasikini.
Jafo pia aliitaka Bodi kuhakikisha inaimarisha taasisi za shirika hizo kama hospitali ya Tumbi, chuo na shule zilizo chini ya Shirika ili ziendelee kufanya vizuri na kuwanufaisha wananchi wanaozunguka shirika na watanzania kwa ujumla.
Jafo pia alilipongeza Shirika hilo kwa Hospitali ya Tumbo kuja na ubunifu wa kutengeneza maji tiba(drip) ambao umesaidia kuipunguzia serikali gharama za kuagiza maji hayo sambamba na shule ya sekondari kibaha na Chuo cha Ufundi (TDF) kufanya vizuri.
MKuu wa wilaya ya Kibaha, Assumpter Mshama ambaye pia ni makamu mwenyekiti wa Bodi alisema changamoto inayofanya Shirika hilo kutosonga mbele ni ufinyu wa bajeti.
Mshana ambaye pia alikuwa ni mjumbe wa bodi iliyopita aliomba serikali kuhakikisha inatoa majibu ya kuruhusu au kukataa maandiko mradi ambayo Shirika inaomba kutekeleza kwa haraka ili kuweza kusonga mbele.
“Tumekuwa tunakwama sana kutokana na kuchelewa kwa serikali kutoa kauli ya ndio au hapana katika maandiko mradi ambayo Shirika tumekuwa tukiomba kutekeleza.
“ Unapeleka andiko, mwaka mmoja, miwili hupati jibu lakini tukipata majibu mapema ya kama ndio tuendelee au hapana inakasoro badilisheni hili na lile, au mradi huu haufai kabisa ili kuja na mawazo mengine, hivyo tunawaomba wataalamu wa TAMISEMI kufanyia kazi maandiko tunayowaletea.”
Naye Mwenyekiti wa Bodi, Profesa Chibunda alisema Bodi yake inakwenda kutekeleza maagizo aliyoyatoa na kulifanya shirika liimarike zaidi.
Pia alioamba ushiriki wa karibu wa Shirika katika hospitali ya Tumbi na Shule zake ambavyo kwa sasa viko chini ya Serikali.
“Tunaona kuna haja ya kubadilishwa kwa mfumo wa uendeshaji, tunataka ya shirika kwenye shule, hopitali ya Tumbi ili Shirika liweze kuwekeza.”
Shirika la Elimu Kibaha ni Shirika la umma linalotoa huduma mbalimbali, lililopo Mkoa wa Pwani, lilianzishwa mwaka 1963 kama mradi wa pamoja chini ya wafadhili watano- Serikali ya Tanganyika kwa kipindi hicho kwa upande mmoja pamoja na nchi nne za Kinordic (Dernmark, Norway, Finland na Sweden) kwa upande mwengine.
Kwa kipindi hicho mradi huu ulijulikana kama “Tanganyika Nordic Project” mpaka mwaka 1970 ambapo mradi huu ulikabidhiwa rasmi kwa Serikali ya Tanzania na kuitwa Shirika la Elimu Kibaha. Na kusajiwa chini ya sheria ya Mashirika ya Umma Na.17 ya mwaka 1969, marejeo ya mwaka 2002.
Post A Comment: