Na Woinde Shizza,Arusha
Shirika la CILAO limefungua kesi leo katika Mahakama Kuu ya Tanzania Masijala ya Arusha kumshtaki Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Yustino Ndugai, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Ndanda Cecil Mwambe kufuatia kitendo cha Spika kumruhusu Cecil Mwambe kuendelea kuhudhuria vikao vya bunge aliyakuwa alitangaza kujiuzuru .
Akiongea na waandishi wa habari mkurugenzi mtendaji wa Shirika la CILAO Odero Oder alisema kuwa wameamua kufungua kesi hiyo leo na kuiomba Mahakama kutoa tafsiri kuhusu kitendo cha spika kumrejesha bungeni aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Ndanda Cecil Mwambe wakati alishajihuzuru nafasi yake ya ubunge na uanachama wa Chadema na kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Alisema Shirika la CILAO kabla ya kufungua kesi hiyo, lilikusanya maoni ya watanzania waliofikia 3000 wakipinga kitendo cha Spika kumrejesha bungeni Cecil Mwambe,huku alibainisha kuwa CILAO imefungua kesi hiyo kwaniaba ya watanzania na watu wote wanaopenda utawala wa Sheria katika nchi yetu.
Akiongelea sababu zilizofanya kufungua kwa kesi hiyo kiongozi wa jopo la mawakili waliopeleka kesi hiyo mahakamani wakili msomi John Seka alisema Kwamba Ibara ya 26(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977, inatoa wajibu wa kila raia kuitii Katiba pamoja na Sheria za Jamhuri ya Muungano ambapo Spika wa Bunge, Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Ndanda Cecil Mwambe wanawajibu pia wa kuitii Katiba ikiwemo Ibara ya 71(1)(f) ya Katiba pamoja na kifungu namba 6C(2) na 6C(3) cha Sheria ya Vyama vya Siasa [Sura ya 288 Toleo la Mwaka 2002].
Alisema Kwamba kwa mujibu wa Ibara ya 71(1)(f) ya Katiba na kifungu namba 6C(2) na 6C(3) cha Sheria ya Vyama vya Siasa [Sura ya 288 Toleo la Mwaka 2002], Mbunge atakoma kuwa mbunge endapo atajihuzuru nafasi yake ya ubunge na kuhamia chama kingine kama ambavyo Bw Cecil Mwambe alijihuzuru.
Alibainisha uzoefu wa uendeshaji wa kibunge na kama ambavyo ilishawahi kutolewa ufafanuzi na Spika kwenye kesi ya Abdalah Mtulia, Mwita Mwikabe, Dr. Godwin Mollel, Katani Ahmad Katani na wengine wengi, yanadhihirisha wazi kwamba Mbunge akitangaza kujihuzuru ubunge na kuhamia chama kingine, Mbunge huyo anakoma kuwa mbunge,ambapo hata
Spika alishathibitisha kujihuzuru kwa Mbunge Mwambe na alitoa maagizo ya kusitishwa mshara wa Mwambe baada ya Februari 15, 2020.
Alibainisha kuwa CILAO inaamini Mahakama Kuu itatenda haki katika kutoa tafsiri sahihi ya Katiba na Sheria ya Vyama vya Siasa kama ambavyo kesi yetu imeeleza.
"Shirika la CILAO linawashukuru watanzania wote waliotoa maoni yao kuhusu kupinga kitendo cha Spika kumrejesha bungeni Bw Cecil Mwambe. Tunawashukuru watanzania wote waliotoa maoni na tunaamini Mahakama Kuu itawatendea haki wananchi katika kesi hii muhimu katika kuhakikisha utawala wa Sheria unazingatiwa"alibainisha John
Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la CILAO Odero Oder akiongea na waandishi wa habari hii leo
Post A Comment: