Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega akisisitiz unywaji wa maziwa kwa watanzania katika uzinduzi wa wiki ya maziwa uliofanyika leo jijini Dodoma. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi.
Wadau mbalimbali pamoja na wandishi wa habari wakifuatilia mkutano wa uzinduzi wa wiki ya maziwa uliofanyika Dodoma.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega akizungumza na wadau mbalimbali katika uzinduzi wa wiki ya maziwa uliofanyika jijini Dodoma leo.
Charles James,
SERIKALI imesema itaanzisha kampeni ya kukagua Ofisi za Umma na binafsi ambazo zinatumia maziwa ya unga badala ya maziwa halisi yanayotengenezwa nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega leo jijini Dodoma wakati akizindua wiki ya maziwa nchini ambayo itafanyika hadi Juni 1.
Naibu Waziri Ulega amesema ni jambo la aibu kuona watanzania wakitumia maziwa ya unga na kuacha yale yanayotengenezwa na watanzania wenzao jambo ambalo amesema siyo la kizalendo.
Amesema hakuna shida ya maziwa nchini kiasi cha wananchi kutumia maziwa ya unga na kueleza kwamba Tanzania inazalisha Lita bilioni tatu kwa mwaka ambayo inatosheleza.
“ Leo ukipita katika ofisi za Serikali karibu zote zinatumia maziwa ya kopo yanayozalishwa nje ya nchi, huu sio uzalendo, lazima tuwe wazalendo kwa kuanza kupenda vya kwetu, ifike hatua tuone aibu kwa ofisi tena za serikali kunywa maziwa ya kopo.
Kama Taifa tukaamua kwa pamoja kunywa maziwa yetu yanayozalishwa hapa nchini tutakua siyo tu tunachangia pato la Taifa kwa kukuza uchumi bali tutaondoa umaskini kwani wafugaji na wauzaji wengi wa maziwa watafanya biashara kwa wingi," Amesema Ulega.
Amesema sekta ya maziwa inachangia asilimia 1.2 ya pato la Taifa na kusisitiza unywaji wa maziwa kwa wingi utasaidia kutimiza ndoto ya Rais Dk John Magufuli kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025.
Naibu Waziri Ulega amesema serikali imekua ikiangaika kutafuta vyanzo vipya vya mapato lakini kama fursa ya biashara ya maziwa itatumika vizuri basi Tanzania itapiga hatua kubwa sana kiuchumi.
" Niwasihi watanzania wenzetu kuanza kutumia vya kwetu, unywaji wa maziwa kwa wingi utachangia sana ukuaji wa uchumi wetu, Shule ya Serikali na binafsi zinapaswa zianzishe utaratibu wa watoto wetu kunywa maziwa ili uwe kama Utamaduni wetu," Amesema Naibu Waziri Ulega.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi amesema unywaji wa maziwa unachangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha afya na kutoa rai kwa wananchi wa Dodoma na watanzania kwa ujumla.
" Nitoe rai kwa watanzania kuwa na utaratibu wa unywaji maziwa, hii itasaidia kukuza uchumi wa Taifa letu lakini pia itachangia uimara wa afya zetu," Amesema DC Katambi.
Post A Comment: