Mkazi wa kijiji cha Seke Ididi wilayani Kishapu mkoani shinyanga Lucia Lukenya (42) kwa tuhuma ya kumuua na kisha kumzika mwanae mwenye jinsia ya kiume mwenye umri wa siku mbili.

Akizungumza na Waandishi wa habari Leo Mei 28 mwaka huu Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo Aprili 19 Mwaka huu katika kitongoji cha Wizunza wilayani humo baada ya kujifungua.

Alisema kuwa Lucia alikamatwa na jeshi la polisi Mei 26 mwaka huu majira ya saa 12 baada ya wananchi wa kitongoji hicho kubaini hana mtoto aliyejifungua salama ndipo walipoamua kutoa taarifa kwa jeshi la Polisi.

"Uchunguzi wa awali unaonesha kuwa Mtuhumiwa alijifungua mtoto huyo tarehe 17/4/2020 na kisha kumuua Tarehe 19/4/2020 na kuamua kumzika peke yake katika eneo la shule ya msingi Ididi majira ya saa 12 jioni wakati mvua ikiendelea kunyesha ili watu wasimuone,"alisema Magiligimba.

Kamanda Magiligimba alifafanua kuwa Mabaki ya mwili wa marehemu yalipatikana tarehe 26 mwaka huu katika kaburi alilozikwa na Mtuhumiwa huyo na kukabidhiwa kwa ndugu zake kwaajili ya taratibu za mazishi.

Ameongeza kuwa chanzo cha mauaji hayo ni ugumu wa maisha baada ya kutelekezwa na mwanaume aliyempa mimba na kutoa wito kwa wananchi mkoani humo hususani wanawake kuacha kukatisha uhai wa watoto kwa visingizio vya   kutelekezwa na badala yake wafike katika madawati ya jinsia yanayopatikana katika vituo vya polisi ili kupata ufumbuzi.

Amesema baada ya kukamilika kwa upelelezi mshitakiwa atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.


Share To:

Post A Comment: