Kiongozi wa Madhehebu ya Shia Tanzania, Azim Dewji
ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Amani Mkoa wa Dar es Salaam, amemtia moyo
Rais John Magufuli kwa msimamo wake katika janga la virusi vya corona na
anavyoongoza nchi akimtaka asivunjike moyo kwani baadhi ya Watanzania
wanampinga.
“Nimewiwa kumzungumzia Rais Magufuli na kumtia
moyo, kwani manabii wengi hawakubaliki nyumbani. Mimi natambua juhudi zake na
ameidhihirishia dunia hata Waafrika wana msimamo kwa yale wanayoyasimamia,”
alisema Dewji juzi alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Alisema Sikukuu ya Idd el-Fitr imefanyika kwa
utulivu wa ajabu na amani, jambo ambalo hakulitarajia wakati huu wa mapambano
dhidi ya virusi vya corona ambapo baadhi ya nchi zimefungia watu ndani.
“Unajua watu wengi wanachukulia mambo kirahisi tu
kwa mtindo poa lakini hili la sikukuu ya Idd el Fitr kufanyika kwa amani na
utulivu ilihali kuna janga la virusi vya corona ni la kumshukuru Mungu kumpa
ujasiri Rais Magufuli kuendesha nchi kwa busara na sio kwa shinikizo la nchi za
nje,” alisema.
Dewji alisema kuwa Rais Magufuli ni kiongozi
hodari na ni viongozi wachache wanaoweza kuamua mambo kama hayo kwa ujasiri na
upekee, kwani jambo la kutofungia wananchi na kuwaacha watoke wakatafute riziki
huku wakichukua tahadhari ni jambo jema ambalo baadhi ya nchi nao wameliiga.
Alisema tatizo kubwa barani Afrika na hata
Tanzania ni watu wengi kutowathamini viongozi wao pale wanapozungumza hadi
wasikie mzungu na kusema huo ni mtazamo hasi unaopaswa kuachwa mara moja.
“Tatizo la Waafrika wengi hatuthamini viongozi
wetu wanapozungumza hadi tumsikie mzungu. Rais Magufuli aliliona mapema akasema
nyumba za ibada zisifungwe watu waendelee kumwabudu Mungu wao kwa kuchukua
tahadhari. Leo tumeona nchi nyingine mfano Marekani, Rais Donald Trump naye
kasema nyumba za ibada zifunguliwe ili watu waabudu,”alisema Dewji katika
mazungumzo yake.
Post A Comment: