Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewaasa wajasiliamali Mkoani Rukwa kutotaja ugonjwa wa Corona (Covid-19) kama kikwazo cha kushindwa kununua kitambulisho cha mjasilimali kwa mwaka huu 2020, kwani wananchi wa Tanzania walihimizwa kuendelea kuchapa kazi na Rais Dkt. John Pombe Magufuli hali ambayo ni tofauti na nchi nyingine ambapo wananchi wake walikuwa wamefungiwa.
Mh. Wangabo amekataza vitambulisho hivyo kuuzwa rejareja kwani jambo hilo huzalisha wadaiwa (defaulters) na hivyo kuwataka wahusika kuviuza vitambulisho hivyo kwa fedha taslimu na kisha fedha hizo ziwasilishwe kwenye akaunti ya Katibu Tawala wa Mkoa ili zifikishwe Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwaajili ya kutumika katika maendeleo ya nchi.
“Kwahiyo fedha zitolewe kabla ya kupewa kitambulisho lakini kusiwe na kisingizio cha Covid – 19, kwamba mzunguko wa fedha, sijui nini, hiki ni kitambulisho kinachomtambulisha mjasiliamali ili asipate bugudha yoyote, vinginevyo ukisema kwamba huwezi, watawabugudhi , kwa namna wanayoona wao na kwa sheria zao, kwasababu hawakutambui wewe kama mjasiliamali mdogo, wewe unajitambua lakini hutambuliki, Mheshimiwa Rais amekupa heshimu ya kukutambua kuwa wewe ni mfanyabiashara mdogo, ukivaa kitambulisho chako unakwenda nchi nzima,” Alisema.
Aidha, Mh. Wangabo alitaja changamoto kadhaa zilizokwamisha zoezi la kwanza la uuzaji wa vitambulisho hivyo ikiwemo usimamizi na ukosefu wa Kanzi data ya wafanyabiashara wadogo pamoja na ucheleweshaji wa kuweka mapato kwenye akaunti ya Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) hali iliyopelekea kuchelewa kwa taarifa, hivyo kuwaonya wale wote watakaochelewa kuweka fedha hizo kwenye akaunti ya RAS.
Mh. Wangabo ametoa kauli hizo wakati akikabidhi vitambulisho 3,000 vya awamu ya kwanza kwa wakuu wa wilaya tatu za mkoa wa Rukwa ambapo kwa mwaka 2019, Mkoa wa Rukwa ulipokea vitambulisho 55,000 na kuuza vitambulisho 32,028 ambavyo ni sawa na asilimia 58.2 na hivyo kukusanya shilingi 640,560,000/= na mwaka huu mkoa unatarajia kupokea vitambulisho 25,000.
Akitoa neno la shukrani Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda alimuhakikishia mkuu wa Mkoa kuwa maelekezo yanayotolewa na serikali hayahitaji kujadiliwa zaidi ya kuyatekeleza na kuongeza kuwa changamoto zozote watakazokumbana nazo watakuwa tayari kukabiliana nazo ili kuhakikisha uchumi wa nchi unaimarishwa na wanachi wenyewe.
“Mimi nimepokea na nitakwenda kutekeleza kwasababu maelekezo ya serikali sisi watendaji tulioko huku chini tunayapokea na kuyatekeleza, kwahiyo changamoto zozote ambazo zitajitokeza, tutakabiliana nazo kwasababu mimi pia naamini, uchumi wa nchi hii utajengwa na wananchi wenyewe, kwahivyo hii ni sehemu ya wananchi katika kuokoa na kuimarisha uchumi wa nchi yao kwa faida yao, kwahiyo ni suala ambalo tunaipongeza serikali na wajasiliamali wadogo wana nafasi ya kuchangia kwenye uchumi wa nchi yao,” Alisema.
Kwa awamu ya Kwanza, Manispaa ya Sumbawanga wamepewa vitambulisho 800, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga wamepewa vitambulisho 800, Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi wamepewa vitambulisho 800 na Halmashauri ya Wilaya ya kalambo Wamepewa vitambulisho 600 na hivyo kusubiri awamu ya pili ya ugawaji huo ambao utahusisha vitambulisho 22,000 kwa halmashauri zote nne za mkoa huo.
Post A Comment: