MKAZI wa Wilaya ya Babati Mkoani Manyara, Idd Sulle amehukumiwa kwenda jela miezi mitano kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa ya shilingi 120,000.
Hakimu mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Babati, Victor Kimaro alitoa hukumu hiyo jana mjini Babati kwenye mahakama hiyo.
Hakimu huyo alisema mahakama hiyo inamtia hatiani Sulle kwenye kesi hiyo ya jinai namba CC 92/2020 baada ya kuridhika na ushahidi uliowasilishwa na wakili wa Takukuru Evelyine Onditi.
Hakimu Kimaro alisema hata hivyo, washtakiwa wengine Ezekiel Thamahandi na Basil Umbayda waliachiwa huru baada ya ushahidi dhidi yao kutokidhi misingi ya kosa la jinai.
Hakimu huyo alisema washtakiwa hao watatu walikuwa mawakala wa kutoza ushuru wa mazao na wakaomba rushwa ya shilingi 120,000.
Alisema washtakiwa hao walikuwa mawakala wa kutoza ushuru katika kizuizi cha Sinai na Kampala wilayani Babati.
Alisema washtakiwa hao waliomba rushwa hiyo Machi 25 mwaka huu kutoka kwa mfanyabiashara wa mazao mkazi wa Singida.
Alisema waliomba rushwa hiyo kwa mfanyabiashara huyo aliyekuwa anasafirisha mazao ya mchele, vitunguu na viazi vitamu kwenda jijini Arusha.
Alisema baada ya kuombwa rushwa ya shilingi 120,000 mfanyabiashara huyo alitoa taarifa kwa maofisa wa Takukuru ambao waliweka mtego na kukamatwa washtakiwa.
"Mahakama baada ya kupitia ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka na utetezi ilimkuta Sulle na hatia na kuwaachia huru Umbayda na Thamahandi," alisema.
Hata hivyo, Mkuu wa Takukuru wa mkoa wa Manyara, Holle Joseph Makungu alitoa rai kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa kila wanapodaiwa rushwa kupitia namba ya dharura ya 113 au kufika ofisini kwao.
Makungu alisema jukumu la kupiga vita rushwa ni la kila Mtanzania hivyo watoe taarifa pindi wakiombwa rushwa kwani rushwa ni adui wa haki.
Post A Comment: