Na. Angela Msimbira CHAMWINO
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo ameridhishwa na kasi ya ujenzi unaoendelea katika Hospitali ya Uhuru inayojengwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma.
Waziri Jafo ameyasema hayo leo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Uhuru ambayo inatarajiwa kukamilika ifikapo Mei, 2020.
Waziri Jafo amesema pamoja na changamoto zote zilizojitokeza za mvua ambayo imeathiri kazi kwa kiasi kikubwa lakini bado SUMA JKT imeendelea kufanyakazi usiku na mchana kuhakikisha kazi inakamilika kwa muda uliyopangwa.
“Nimeridhika na kasi ya ujenzi unaoendelea katika Hospitali ya Uhuru na hasa nimefurahishwa na utekelezwaji wa maagizo yangu niliyoyatoa ya kuongeza nguvukazi, sasa naona kuna nguvukazi ya watu 300 ambao ni tofauti na awali walikuwepo 100” ameeleza Waziri Jafo.
Ameutaka uongozi wa Suma JKT kuhakikisha wanasimamia ujenzi wa Hospitali hiyo ili kuweza kukamilisha kazi hiyo kwa wakati uliopangwa.
Waziri Jafo ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino kuhakikisha vifaa vya ujenzi vinanunuliwa kwa wakati ili mkandarasi asipate shida ya kukamilisha ujenzi wa Hospitali hiyo katika kipindi kilichopangwa.
Naye Mhandisi wa SUMA JKT Omary Kabalangu amesema kuwa tayari wameongeza kikosi kazi kwa ajili kuongeza nguvu ya ujenzi na watahakikisha wanafanyakazi usiku na mchana ili kukamilisha ujenzi huo katika muda uliopangwa na Serikali.
Aidha mradi wa Hospitali ya uhuru inajengwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Mkoani Dodoma na unagharimu shilingi bilioni 3.99. Fedha za ujenzi zilizotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli, Fedha ambazo zilitakiwa kutumika katika sherehe za maadhimisho ya siku ya uhuru wa Tanganyika Desemba, 9 mwaka 2018ambazo zilitolewa na kammpuni ya simu ya Airtel kama gawio
Post A Comment: