Aliyekuwa mstahiki meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Alex Kimbe akionesha barua ya gari alilokuwa akitumia

Aliyekuwa mstahiki meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Alex Kimbe akiwaaga watumishi 
Wanahabari wakipiga picha meya Kimbe wakati kuingia kwenye gari yake binafsi 
Kimbe akihojiwa na wanahabari 
Watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa wakimsikiliza Kimbe 
......................


ALIYEKUWA mstahiki meya wa  Halmashauri ya  Manispaa ya  Iringa  kupitia  chama cha  Demokrasia na maendeleo (CHADEMA) Alex  Kimbe amekabidhi  ofisi  kwa  mkurugenzi wa Halmashauri  hiyo Himid Njovu ikiwa ni pamoja na kufanya kikao cha mwisho na  watumishi  wote wa Halmashauri hiyo  akiwaleza  kuwa hana kinyongo  ataendelea  kutoa ushirikiano kwa  maendeleo ya wananchi .

Akizungumza  wakati wa kikao chake na  watumishi hao  kilichofanyika  kwenye ukumbi wa Halmashauri  hiyo Kimbe  alisema kuwa   baadhi ya maeneo  ambayo  walifanya mchakato kama huo wa  kumwondoa mstahiki meya kama Dar es Salaam hadi leo  vikao  vya baraza la madiwani na vikao  vya kamati mbali mbali  havifanyiki  kutokana na meya  aliyeondolewa  kugoma kukabidhi ofisi  ila  yeye ameona ni hekimu  kuwa  kuepusha mivutano ya kisiasa yenye lengo la kukwamisha maendeleo na  kuamua kutumia busara  yake  kukabidhi ofisi kama alivyotakiwa  kufanya hivyo .

'' Ikitokea  vikao  vya  baraza la madiwani havifanyiki  katika Halmashauri   husika  ni wazi maendeleo  hayajakuwepo  maana  pasipo  vikao  vya madiwani hakuna  kinachoendelea kwenye Halmashauri kwa hiyo  nimefikiria  kwa kina mahitaji ya  wananchi wetu wa Manispaa ya  Iringa na sasa barabara  nyingi zimeharibika  nawananchi wanahitaji  kutatuliwa  kero  hizo za ubovu wa miundo mbinu na nyingine  ambazo zote zinahitaji vikao vya madiwani vifanyike  kwa  hilo  nimeona  ni  vema busara itumike ili  maendeleo yafanyike na kutolewa kwwangu kusiwe mateso kwa  wananchi wasio na hatia nimeamua  kuja kukabidhi ofisi mambo yaendelee '' alisema Kimbe 

Alisema  kuwa  ili  shughuli mbali mbali za kimaendeleo  ziweze  kufanyika katika halmashauri  hiyo ya Manispaa ya Iringa ni lazima  madiwani wakae na maamuzi yafanyike  ya  kutenga bajeti ya shughuli za kimaendeleo  na kuendelea na migogoro ya  kugoma kutoka madarakani si  tu  unawakomesha  madiwani wa chama cha mapinduzi (CCM) ambao  walihusika kumtoa katika nafasi yake ila wanaoteseka ni  wananchi wa Manispaa ya Iringa.
Kimbe  alisema kuwa  kwa lile tukio  lililofanyika juzi machi 28  la kumtoa madarakani yeye  kwa upande wake ameridhika nao na ameona  si sahihi  kung'ang'ania nafasi hiyo ambapo kimsingi ni nafasi ambayo alipewa na madiwani wenzake kuwasimamia ili  kuongoza Halmashauri hiyo na sio nafasi ambayo wananchi  walimchagua maana nafasi aliyoomba kwa  wananchi ni nafasi ya  udiwani wa kata ya Isakalilo ambao ataendelea nao hadi hapo muda wake  utakapokoma miezi michache   ijayo .

'' Kwa  kuwa  nimeridhika na mchakato wa  kunitoa uliofanyika ambao nilipigiwa  kura 14  za ndio kati ya kura 26 za wajumbe   wote  pamoja na kuwa  kura za kunitoa zilipaswa  kuwa kuanzia 17   ila sina  kinyongo  chochote na kutolewa  kwangu  kwa  sababu wakubwa  walitaka  nitoke ili  kujifurahisha na nafsi zao sitaki  kuwakwaza  nimetoka  na leo nimeona  nije kuwatia moyo  watumishi  wenzangu kwa ushirikiano mzuri  mlionesha  kipindi nikiwa meya wa Halmashauri ya Manispaa ya  Iringa na nawaombeni mzidi  kuwajibika kwa maslahi mapana ya wananchi wa Manispaa ya  Iringa '' alisema Kimbe 

Kuwa  kwa upande  wake  ushauri ambao  alikuwa  akiutoa kwa Halmashauri  ataendelea  kuutoa na ataendelea  kuonekana katika  viwanja vya manispaa ya Iringa kama  diwani wa kata ya Isakalilo na pale mkurugenzi wa Halmashauri   hiyo na watumishi wengine watakapohitaji msaada wake wa kimawazo kwa  ajili ya maendeleo ya  wana Iringa atautoa na watumishi wasiogope  kumuomba  ushauri  pale inapohitajika kufanya  hivyo .

Aidha  alisema kuwa  kwa  upande wake  alikuwa na ndogo   kubwa za kimaendeleo katika mji wa Iringa na miongoni mwa mikakati yake kupitia baraza la madiwani  walikuwa  wakitarajia  kuwa na vitengo uchumi vingi kama ujenzi wa  utawala  ,jengo la biashara  Tembo Bar  na  kwa  kuwa  sheria  inamtaka yeye kama diwani  kutoa ushauri wake kwenye  baraza la madiwani ataendelea  kufanya hivyo kwa faida ya wananchi wa Iringa .
Alisema  jambo kubwa ambalo  lilimsukuma  kuagana na watumishi hao leo  ni kutokana na ushirikiano mkubwa ambao alionesha   wakati  wote   wa  utawala  wake kama mstahiki meya wa Halmashauri  hiyo  toka  alipochaguliwa  miaka mitano iliyopita  kuongoza nafasi hiyo .

'' Nawaomba  sana   watumishi wote  wa Manispaa ya Iringa  msijisikie  vibaya kuondolewa kwangu madarakani  naomba  mfanye kazi ya  kuwatumikia wananchi kwa  moyo wa kujituma  zaidi kwani kuondoka kwangu  kusiwe mwanzo wa watumishi  kuvunjika moyo  wa kufanya kazi ''

Kimbe  alisema  anachojivunia kwa  utawala wake kama Mstahiki meya wa Manispaa ya Iringa kwa  miaka  yote  minne halmashauri  hiyo imekuwa ikipata  hati  safi na hata siku moja   haikupata kufanya vibaya katika ukusanyaji wa mapato yake  wala katika suala  la usafi  wa mji na anatamani  wanaobaki  kwa kipindi  hiki  kifupi  kulinda  heshima  hiyo  aliyoiacha.

Alisema  kuwa  akiwa Meya   Halmashauri  hiyo  imepata  kujenga  shule  nyingi za sekondari pia ujenzi wa Hospitali ya wilaya ya Frelimo ,vituo  vya afya na miradi mingine mingi ya kimaendeleo ambayo imefanyika kwenye Halmashauri hiyo kama mradi mkubwa wa stendi ya mabasi Igumbilo ,soko la Kisasa la Mlandege pia  matokeo ya mitihani ya  darasa la saba kitaifa Manispaa ya  Iringa imeendelea  kufanya  vizuri  sana .

'' Natambua mazuri  mengi  yamefanyika ila kuondolewa kwangu  hakuna baya nilillolifanya  ila  wakubwa  hawakutaka Manispaa ya Iringa  kuwa na meya wa Chadema  kwa  sababu ambazo  wanazijua wao ila hakuna sababu nyingine  ambazo zilifanya nitoke madarakani  ila nachojivunia dunia yote  inajua haya na kuondoka kwangu hivyo  heshima yangu  imeongezwa thamani na watalawa  waliotaka  nitoke madarakani ila  wananchi wanatambua mimi bado ni meya  wa mioyo yao  leo  nimekabidhi ofisi na gari naingia kwenye gari langu kuendelea na majukumu yangu ya udiwani na nitagombea tena udiwani Isakalilo katika uchaguzi mkuu  ujao ''

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya  Iringa Himid Njovu alimpongeza Kimbe kwa maneno yake mazuri ya  busara  na kuwa anamkaribisha kuendelea  kutoa ushirikiano kwa nafasi yake ya  udiwani katika kuongoza Halmashauri  hiyo
Share To:

Francis Godwin Mzee wa matukiodaima

Post A Comment: