…………………………………………………………………………
Miili ya wafanyakazi watano wa Shirika la Reli Tanzania – TRC waliofariki kutokana na ajali ya treni ya uokoaji kugongana na Kiberenge katika eneo lililopo kati ya stesheni ya Mwakinyumbi na Gendagenda mkoani Tanga imeagwa rasmi katika hospitali ya Lugalo jijini Dar es Salaam leo Machi 24. 2020.
Zoezi hilo la kuaga miili ya mashujaa hao limesimamiwa na uongozi na wafanyakazi wa TRC na kuhudhuriwa na ndugu wa marehemu, Katibu wa Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndugu Humphrey Polepole, pamoja na wadau wengine wa TRC wakiwemo Benki ya CRDB, TIB, NBC, wadau wa reli kutoka TAZARA, YAPI MARKEZI pamoja na wadau kutoka chuo cha DIT na Meneja kutoka kampuni ya Wasafi Classic Baby (WCB) Ndugu Hamis Taletale maarufu kama Babu Tale.
Mkurugenzi mkuu wa TRC ndugu Masanja Kungu Kadogosa amesema kuwa amesikitishwa na tukio hilo kwani TRC pamoja na Serikali kwa ujumla imepoteza nguvu kazi ambayo ilikuwa ikitoa mchango mkubwa katika Shirika na Serikali.
“Kiukweli nimeumia sana na sijawahi kuumia kama hivi, ila sisi ni wanadamu na chochote kitakachotokea huwa ni mipango yake Mungu, kinachotakiwa ni kushukuru na kuwa na subira” alisema Ndugu Kadogosa.
Aidha, Ndugu Kadogosa amesisitiza kuwa uchunguzi wa chanzo cha ajali hiyo utafanyika kupitia tume huru itakayoundwa hivi karibuni kama lilivyoagizwa na Naibu waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi Mhe. Atashasta Nditiye alipotembelea eneo la ajali hivi karibuni ambapo tume hiyo itatakiwa kutoa majibu ndani ya siku saba tangu kuundwa kwake.
Kadogosa ameongeza kuwa majibu ya uchunguzi huo yatabaini chanzo cha ajali na lengo ni kuepusha madhara kama hayo yasijirudie tena kwani kazi za reli bado zinaendelea na juhudi za kuwalinda wafanyakazi zinatakiwa kufanywa kwani wao ndio nguvukazi ya shirika na taifa kwa ajili ya kuleta maendeleo kupitia miundombinu ya reli.
TRC imesimamia shughuli zote za mazishi nyumbani kwa marehemu hao ikiwemo katika usafirishaji wa miili, chakula, pamoja na kutoa na kupokea salamu za rambirambi kutoa kwa wadau mbalimbali waliojitokeza na katika maombolezo hayo.
Aidha Ndugu na jamaa wametoa shukrani kwa uongozi na wafanyakazi wa TRC kwa kuweza kushiriki nao bega kwa bega katika kuhakikisha wanawahifadhi wapendwa wao, mwili wa Marehemu Ramadhani Gumbo unazikwa leo mjini Bagamoyo, huku miili ya marehemu iliyobaki itasafirishwa kwa ajili ya mazishi siku ya Jumatano na Alhamisi.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: