Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi akizungumza na kamati tendaji ya viongozi wa serikali za wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu (Tahliso) katika mkutano wa pamoja jijini Dodoma.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi akiwa katika picha ya pamoja na kamati tendaji ya viongozi wa serikali za wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu nchini (Tahliso).
VIJANA nchini wametakiwa kuwa wabunifu katika kufikia ndoto zao na siyo kukaa vijiweni wakilalamikia ugumu wa maisha na kusubiri serikali iwafanyie kila kitu.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi alipokua akizungumza na kamati tendaji ya viongozi wa serikali za wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu (Tahliso) jijini Dodoma.
Katambi amewataka viongozi hao ambao wanaongoza kundi kubwa la vijana wasomi kuwahimiza wenzao kuwa wabunifu lakini pia kuwa mabalozi wa mambo makubwa ya kimaendeleo yaliyofanywa na serikali ya awamu ya tano.
Amewataka kutoyumbishwa na maneno yanayosemwa na wanasiasa nchini na badala yake kama vijana viongozi wawe wanatembelea miradi ya serikali na kujionea wenyewe.
" Nyinyi ni wasomi tena ni viongozi hampaswi kukaa tu nakusikiliza maneno ya wanasiasa. Someni na mtembelee miradi inayofanywa na serikali ndipo mtaona ni kwa kiasi gani hawa wanasiasa wasio na hoja wanavyodanganya watanzania.
Leo Dodoma inajengwa stendi ya mabasi kubwa na ya mfano Afrika Mashariki, soko la kisasa linajengwa, uwanja wa Kimataifa unajengwa lakini pia kuna reli ya kisasa ya mwendokasi, hii yote ni kazi iliyotukuka ya Rais Dk John Magufuli, siyo Dodoma tu kila kona ya Nchi yetu ardhi inalia kwa namna ambavyo miradi ya kila aina kuanzia Afya, Nishati, Miundombinu, Elimu inavyotekelezwa," Amesema Katambi.
Amewataka viongozi hao kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha umoja nchini pamoja na kuhamasisha vijana kukimbilia fursa mbalimbali badala ya kukaa kijiweni na kuilaumu serikali.
DC Katambi pia amewasisitiza viongozi hao kuungana na serikali katika kuhamasisha wananchi kuchukua tahadhari ya ugonjwa wa Corona ikiwa ni pamoja na kutumia vitakasa mikono pamoja na kuepuka misongamano ya watu isiyo ya lazima.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tahliso, Peter Niboye amemshukuru DC Katambi kwa kukubali kuwa mgeni rasmi kwenye mkutano wao huo sambamba na kutoa mada ya uongozi, uzalendo.
" Tunashukuru sana kwa mada ulizotoa naamini sisi sote tutatoka hapa tukiwa tumeingiza kitu kipya kichwani, tunashukuru pia kwa mualiko wako uliotupa wa kutembelea miradi yote ya kimaendeleo inayotekelezwa kwenye Jiji lako, na tunakuahidi tutakua mabalozi wa kueleza mafanikio ya serikali yetu," Amesema Niboye
Post A Comment: