TAASISI ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) mkoani Manyara inawashikilia mawakala watatu wa kukusanya ushuru wa mazao katika Halmashauri ya Babati Mjini na Halmashauri ya Babati vijijini.
Hayo yameelezwa leo machi 27,2020 na mkuu wa Takukuru mkoani hapa Holle Makungu wakati akitoa taarifa ya kukamatwa kwa mawakala hao kwa waandishi wa habari.
Makungu amewataja waliodakwa na rushwa kuwa ni Iddy Sulle wa kituo cha kazi kizuizi cha Sinai kilichopo Halmashauri ya Mji wa Babati, Ezekia Thanahandi wa kizuizi cha Kampala kilichopo Halmashauri ya wilaya ya Babati na mwingine ni Basil Aloyce ambaye kituo chake cha kazi ni Sinai kilichopo Halmashauri ya Mji wa Babati.
Amesema mawakala hao waliomba rushwa ya sh. 120,000 kutoka kwa mfanyabiashara wa mazao jina limehifadhiwa kwa sababu za kiuchunguzi.
Amesema waliomba rushwa hiyo kwa mfanyabiashara wa mazao aliyekuwa akisafirisha mchele, vitunguu na viazi mviringo kwa gari kutoka Singida kwenda Arusha Machi 25, 2020.
"Awali mfanyabiashara huyo alipita kizuizi cha Kampala kilichokuwa kimefunguliwa bila ya kuwepo kwa wakusanya ushuru , hata hivyo gari hilo lilipofika kituo cha Sinai lilizuiliwa,"Alisema Makungu
Aidha amesema baada ya muda mfupi Sulle na Thanahandi kutoka kizuizi cha Kampala walifika eneo lile na kuchukua hati za kusafirishia mazao hayo.
Ameeleza kuwa vijana hao walimtaka mwenye mazao afuate nyaraka hizo katika kizuizi cha Kampala Machi 26,2020.
"Mfanyabiashara huyo alitii agizo hilo na kulipopambazuka alifuata nyaraka zake kizuizi cha Kampala , ndipo alipopewa sharti la kutafuta 120,000 ili aweze kuwekewa sahihi kwenye nyaraka zake ili aweze kuendelea na safari ya Arusha,"Alieleza
Mtaalamu huyo wa kupambana na rushwa alisema mfanyabiashara huyo hakuridhika ndipo akatoa taarifa Takukuru, uchunguzi ukafanyika kujiridhisha kuhusu madai hayo kisha mtego ukaandaliwa ambazo ndizo ziliwafanya watuhumiwa kukamatwa wakiwa wanajipongeza kwa vinywaji katika Baa ya Mandosi eneo la Dareda kati.
"Ukiacha kucheleshwa kwa sababu za rushwa kwa mfanyabiashara huyo baadhi ya mazao kama vitunguu na viazi vilivyokuwa vinasafirishwa vimeharibika.
Makungu alifafanua kuwa pamoja na watuhumiwa kufikishwa mahakamani watawajibika kwa hasara hiyo ili liwe fundisho kwa wengine.
Amewataka wakurugenzi wa Halmashauri kuweka mawakala waadilifu katika vizuizi vyote au ikiwezekana watumishi wa Halmashauri ili kuwaondolea usumbufu wananchi wanaofanya shughuli zao halali na kudhibiti upotevu wa mapato unaofanywa na baadhi ya mawakala wasio waadilifu.
Naye mkuu wa dawati la elimu kwa umma mkoani hapa Sultan Ng'aladzi amesema kuwa, mawakala hao wamefanya kosa chini ya kifungu cha 15 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa ya mwaka 2007.
Ofisa huyo amesema wamekuwa wakitoa elimu kwa mashirika na taasisi kuhusu mapambano juu ya rushwa na kwamba wataenda kutoa elimu ya kupambana na kuzuia rushwa kwa mawakala ili waache uhalifu huo na wawe waadilifu.
Post A Comment: