Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
TAASISI ya kuzuia na kupambana na Rushwa [TAKUKURU]mkoa wa Dodoma inatarajia kumfikisha mahakama Kaimu katibu wa tume ya utumishi wilayani Bahi Adam Richard (49) kwa tuhuma nne ikiwemo ya kuomba rushwa ya shilingi yazidi ya shilingi milioni 1 kutoka kwa walimu wanne ili awasaidie katika mchakato wa kupandishwa vyeo.
Akizungumza na Waandishi wa habari leo mkuu wa TAKUKURU mkoani wa Dodoma Sosthenes Kibwengo alisema mtumishi huyo amefanya hivyo kinyume na kifungu cha 15 [1]cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa sura ya 329 marejeo ya mwaka 2018 .
“Baada ya kupata taarifa kutoka kwa walimu kwamba mtuhumiwa ana tabia ya kutumia rushwa kama kigezo cha kufanikisha waliompa kupandishwa madaraja ,tulianzisha uchunguzi na tumepata ushahidi kwamba kati ya April,na Juni,2019 mtuhumiwa alitenda kosa hilo na kwa kuwa taarifa tulizopata dhidi yake ni nyingi ,bado uchunguzi wa taarifa zilizosalia unaendelea na ukikamilika atafikishwa mahakamani”alisema.
Aidha Kibwengo alisema TAKUKURU imemfikisha mahakama ya Wilaya ya Kondoa Afisa mtendaji kata ya Thawi Wilayani hapo Bw.Hashim Ally Mohamed [42] na kumfungulia kesi mbili kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa ambapo amefunguliwa shauri la jinai Na.24/2020 mbele ya Hakimu Mwajabu Mvungi .
Kibwengo alifafanua kuwa mtuhumiwa alifanya kosa la kuomba Rushwa ya Tsh 155,000 na kupokea Tsh. 60,000 kutoka kwa mwananchi mmoja ili asimchukulie hatua kwa kosa la mjukuu wa mwananchi huyo kutokwenda shule siku 31 mfululizo .
“Uchunguzi wetu pia umeonesha kuwa mwanafunzi huyo alifuata taratibu zote na amehamia katika shule iliyopo mkoa mwingine ,pili amefunguliwa shauri la jinai Na.26/2020 Mbele ya hakimu Martine Massao kwa kosa la kuomba rushwa Tsh 1,75,000 na kupokea Tsh 80,000 kutoka kwa mwananchi mwingine ili asichukue hatua dhidi yake kwa madai kwamba binti yake hajahudhuria masomo shuleni na alitenda vitendo hivyo vya jinai Februari mwaka huu”alisema Kibwengo.
Katika hatua nyingine kamanda huyo wa TAKUKURU alisema taasisi hiyo kwa kushirikiana na Ofisi ya mashtaka ya Taifa wanatarajia kumfikisha mahakamani mwalimu mkuu wa shule ya msingi Msisi ya jijini hapa David Mdeka(44)mkazi wa Ipagala kwa makosa ya matumizi ya nyaraka kumdanganya mwajiri kinyume na kifungu cha 22 na ubadhirifu kinyume na kifungu cha 28 ,vyote vya sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa na kosa la kughushi kinyume na sheria za kanuni za Adhabu Sura ya 16 marejeo ya Mwaka 2002.
“Uchunguzi wetu umeonesha kwamba Januari ,2015 mtuhumiwa akiwa katibu wa kamati ya shule alighushi mhutasari kuonesha kwamba kamati imeridhia malipo ya Tsh 1,186,000 kwa ajili ya kununua vifaa vya kukarabati choo cha shule ,ambapo alitoa fedha hizo benki na kuzifuja kwani vifaa havikufikishwa shuleni na wala ukarabati haukufanyika“amesema.
Kibwengo alisema wanashirikiana na Ofisi ya Mashtaka ya Taifa kuwafikisha mahakamani Dodoma Robert Mwinje [39]na Nyemo Malenda (20)wote wakazi wa jijini Dodoma kwa makosa matatu ya kula njama ,kughushi, na kuwasilisha nyaraka za uongo ,yote yakiwa ni kinyume cha sheria ya kanuni za Adhabu Sura ya 16 marejeo yam waka 2018.
“Uchunguzi wetu umeonesha kwamba kati ya tarehe 18 na 20 ,Oktoba,2019,Bw.Mwinje ambaye alikuwa mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Dodoma na Bi.Malenda ambaye ni mhudumu wa Ofisi hiyo walighushi barua ya uteuzi wa waomba uongozi ndani ya Chama na huku wakijifanya imetolewa na uongozi wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Dodoma wakaikabidhi kwa uongozi wa mwanachama mmoja kwa hatua huku wakijua kuwa ni uongo”alisema Bw.Kibwengo.
Kibwengo alisema TAKUKURU Mkoa wa Dodoma imeendelea na utekelezaji wa majukumu yake ya kuzuia na kupambana na rushwa kwa kuwashirikisha wananchi huku akiwashukuru kwa kutoa ushirikiano na kuwasihi watumishi wa umma kuzingatia sheria ,kanuni na taratibu za utumishi kwa kujiepusha na vitendo vya rushwa kwani ni adui wa haki .
Post A Comment: