Mwenyekiti wa Mtaa wa Namanyigu kata ya Mshangano Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma ,Abdulqadir Myao akizungumza na wakazi wa mtaa huo kwenye mkutano wa hadhara pamoja na uwasomea taarifa za maendeleo ya mtaa huo
Na Amon Mtega,Songea.
MWENYEKITI wa Mtaa wa Namanyigu kata ya Mshangano Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma,Abdulqadir Myao amewaomba wakazi wa mtaa huo kuendelea kumpatia ushirikiano katika utendaji kazi ili kufanikisha maendeleo kwenye mtaa huo.
Ombi hilo amelitoa wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliyofanyika katika viwanja vya ofisi za mtaa huo ambao ulikuwa kwaajili ya kutoa taarifa za maaendeleo ya mtaa huo.
Myao akitoa taarifa ya maendeleo ikiwemo ya mapato na matumizi yaliyosomwa na mtendaji wa mtaa huo Anusiatha Mapunda amesema kuwa Wakazi wa Namanyigu wakiendelea kutoa ushirikiano kwenye uongozi huo ,maendeleo yatazidi kusongambele.
Mwenyekiti huyo ambaye ni mara yake ya kwanza kuitisha mkutano huo tangu kuchaguliwa kwake amesema kuwa kuna mambo mengi ya kuyafanya kwenye mtaa huo ikiwemo kukamilisha ujenzi wa ofisi ya mtaa pamoja na kuimalisha miundombinu mbalimbali kama ya barabara za kwenye mtaa.
Kwa upande wake mmoja wa wakazi wa mtaa huo Braiton Nchimbi akichangia hoja kwenye mkutano huo amesema kuwa mtaa huo umekuwa ukijitolea katika ufanyaji wa miradi ya maendeleo kimtaa na kikata lakini hakuna hata mradi mmoja mkubwa wa ngazi ya kata uliofanyika kwenye mtaa huo.
“Tunaomba na sisi katika mtaa wetu miradi mikubwa inayohusu kata iweze kutekelezwa na siyo kupendelea mitaa mingine tuu jambo ambalo linatukatisha tamaa wananchi wa Namanyigu”amesema Nchimbi.
Aidha mkazi mwingine Stephano Luoga alilalamikia mambo ya usalama , katika mtaa huo kumekuwepo na wezi (Vibaka)ambao wamekuwa wakiwasumbua wakazi wa mtaa huo kwa kuwaibia vitu vyao kwenye majumba,hivyo aliutaka uongozi uweze kuweka mikakati ya kukabiliana na jambo hilo.
Naye Diwani wa kata ya Mshangano Rotadi Mbawala ambaye naye alihudhuria mkutano huo amesema kuwa kata inatambua changamoto zilizopo na zitaendelea kufanyiwa kazi.
Post A Comment: