Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally ameweka bayana kuwa wanachama wote wanaotarajia kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi Mkuu wana haki sawa, na hakuna mwanachama wa Mwenyekiti wala Katibu Mkuu kama ambavyo baadhi ya wanachama wanavyoanza kuwalaghai wajumbe wa vikao kuwa wametumwa na Mwenyekiti na Katibu Mkuu kugombea.
Amesema kuwa ni vema, kila mmoja ajiandae kueleze sifa zake na kwa nini anadhani anafaa kuliko mwingine na sio kutumia sababu za kilaghai za kutumwa na Mwenyekiti, Katibu Mkuu ama Wazee, kwani anafahamu kuwa Mwenyekiti hana Mgombea yeyote, na yeye (Katibu Mkuu) hana Mgombea kwa kuwa wagombea wote ni wakwao na wanahaki sawa.
Ameyasema hayo leo tarehe 18 Januari, 2020 katika Mkutano Mkuu wa Jimbo la Kigoma Kaskazini wa kupokea taarifa ya kazi ya Mbunge wa jimbo hilo Ndg. Peter Serukamba.
“Wapo watarajiwa wanataka kugombea udiwani, ubunge, ni haki yao, na zipo kanuni na mila zetu, na mojawapo ni wewe kusema sifa zako sio kusema uongo, kusema nimetumwa na Katibu Mkuu kugombea hapa ni uongo, sema sifa zako, kusema nimetumwa na Mwenyekiti (Rais) ni uongo, nimetumwa na wazee, ni uongo, umewafanyaje wazee wakutume, sema sifa zako, una agenda gani, una sifa gani, una uwezo gani, unauzoefu gani, una mipango gani, na unaweza nini sio kusema uongo..”
Amesisitiza kuwa, watu ambao hawana sifa wanajiuza kwa kusema uongo, Mwenyekiti (Mhe. Rais Magufuli) hana Mgombea, wagombea wote ni wa kwake na Mwenyekiti hawezi kuwa na mgombea mmoja, hata yeye wakati anagombea hakusema ametumwa na yeyote ila sifa zake zilimuuza kwa wapiga kura.
Aidha, Katibu Mkuu kabla ya mkutano huo ametembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo mradi wa ujenzi wa barabara ya Chankele - Mwamgongo, upanuzi wa Kituo cha Afya cha Bitale na Kituo cha Utafiti wa mbegu za michikichi cha Kihinga
Ziara hii imeongozwa na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kigoma Ndg. Amandus Nzamba, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa Ndg. Kirumbe Ng’enda, Mkuu wa Mkoa huo Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga, wabunge ni Ndg. Daniel Nsanzugwako, Hasna Mwilima na Peter Serukamba.
Imetolewa na;
Said Said Nguya
Afisa Habari
Ofisi ya Katibu Mkuu
CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)
Post A Comment: