Mkuu wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga Kissa Kasongwa (kushoto) akipata maelezo kutoka kwa Meneja wa Kiwanda cha Mkonge Mwelya kilichopo chini ya Kampuni ya Katani Ltd Nicholaus Noah (kulia). Ni baada ya kufanya ziara Septemba 2, mwaka huu. (Picha na Yusuph Mussa).
Na Yusuph Mussa, Korogwe
Na Yusuph Mussa, Korogwe
MKUU wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga Kissa Kasongwa ameagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) waende Shamba la Mkonge Magunga baada ya baadhi ya wakulima kulalamika kuwa mkonge wao unavunwa, lakini fedha wanapewa watu wengine.
Pamoja na hilo, pia kujua baadhi ya fedha zilipo, kwani kumekuwa na mabishano kati ya Meneja wa Kiwanda cha Mkonge Magunga chini ya Kampuni ya Katani Ltd Abdulrahman Zayumba, na Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika wa Wakulima wa Mkonge Shamba la Magunga (AMCOS) Aliamini Mrutu, kila mmoja akidai anamdai mwenzake fedha, jambo lililosababisha baadhi ya wafanyakazi washindwe kulipwa stahiki zao ikiwemo mishahara.
Akizungumza Septemba 2, 2019 na wafanyakazi wa Kiwanda cha Mkonge Magunga ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kutembelea wafanyakazi kwenye viwanda vya mkonge vya Magoma, Mwelya, Ngombezi, Magunga na Hale, Kasongwa alisema hataweza kukubali kuona baadhi ya watu wananeemeka, huku walio wengi wanateseka.
"Naagiza TAKUKURU, na bahati nzuri upo hapa, uje ufanye uchunguzi kuhusu tuhuma zilizotolewa hapa kuwa baadhi ya watu wanaingiziwa fedha wakati mkonge uliovunwa sio wa kwao. Pia upate uhakika, kati ya Kampuni ya Katani Ltd na AMCOS nani anamdai mwenzake, na kujua fedha hizo zipo wapi na zinafanya nini" alisema Kasongwa.
Kasongwa alisema Wilaya ya Korogwe kwa sasa ndiyo inayofahamika kuwa inaongoza kwa kilimo cha mkonge Tanzania, lakini bado wakulima wake hawajanufaika vya kutosha, hivyo anataka kuona sifa hizo zinaendana na hali halisi kwa maisha ya wananchi kubadilika.
Awali, mmoja wa waliokuwa wafanyakazi wa Shamba la Mkonge Magunga ambaye aliajiriwa na AMCOS, Francis Fute, alisema alipokuwa karani wa kuhesabu mizigo na meta za mkonge, alibaini baadhi ya watu waliopewa kazi ya kubeba mizigo hiyo kupeleka kiwandani kwa ajiili ya kusindikwa, na baada ya malipo wanaopewa fedha ni wengine.
"Mkuu wa Wilaya, Machi, mwaka huu nilipewa kazi na AMCOS kwa ajili ya kuchoma (kuhesabu majani ya mkonge) mkonge. Lakini nilibaini vitu vingi ikiwa ni pamoja na watu waliovuniwa mkonge wao kupunguzwa idadi ya meta zilizovunwa, huku baadhi ya watu wakiingiziwa fedha zisizo za kwao kwenye akaunti zao" alisema Fute.
Awali, Meneja wa Kiwanda cha Mkonge Magunga, Zayumba, bila kutaja kiasi, alisema anawadai AMCOS, huku Mwenyekiti wa AMCOS Mrutu akisema Katani Ltd hadai fedha zozote kutoka kwenye chama hicho.
Mabishano hayo na malalamiko yaliyotolewa na wafanyakazi, ndiyo kumefanya Mkuu wa Wilaya kuwatuma TAKUKURU kupata ukweli juu ya tuhuma za ubadhirifu wa fedha na wizi wa mkonge kwenye kiwanda hicho.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martin Shigela, Agosti 21, mwaka jana, alibadili muundo wa Wakulima wa Mkonge chini ya mfumo wa SISO kwenye mashamba ya Magunga, Magoma, Hale, Ngombezi na Mwelya. Ni baada ya kupata malalamiko kutoka kwa baadhi ya wakulima wa mkonge, kuwa aliyepewa dhamana ya kuwaongoza Kampuni ya Katani Ltd, anachelewesha malipo ya wakulima na wafanyakazi.
Ndipo Shigela kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali akaamua wakulima watajisimamia wenyewe kupitia AMCOS zao kwenye kukata mkonge hadi kuuza, tena kwa mnada. Na Katani Ltd atabaki kama msindikaji tu wa zao hilo, na yeye akilipwa na AMCOS kwa kazi hiyo.
MWISHO.
Post A Comment: