Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia sera, bunge, kazi, vijana, ajira na watu wenye ulemavu Jenista
Mhagama (wa tatu kutoka kulia waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe
walioshiriki katika warsha ya siku moja ya wadau kuhusu ushiriki wa Watanzania
katika miradi ya kimkakati Mkoani Dodoma. Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma
Dkt. Bilinith Mahenge.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera,
Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu Jenista Mhagama amefungua
warsha ya siku moja ya majadiliano ya wadau kuhusu ushiriki wa Watanzania
(Local content) katika sekta ya uziduaji mkoani Dodoma.
Warsha hiyo imewakutanisha pamoja
wawakilishi zaidi ya 100 wa makundi mbalimbali kutoka Wilaya zote za Mkoa wa
Dodoma ili kujadili mikakati na maendeleo ya utekelezaji wa dhana ya ushiriki
wa Watanzania katika fursa za miradi ya kimkakati ikiwemo mradi wa Bomba la
Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Hoima nchini Uganda kwenda
Tanga, Tanzania na sekta ya madini kwa ujumla.
Akizungumza wakati wa kufungua warsha hiyo leo Agosti 26, 2019
katika ukumbi wa Kilimanjaro Hazina Mjini Dodoma Waziri Mhagama aliwataka
viongozi wa maeneo ambako bomba litapita wawahamasishe wananchi kuchangamkia
fursa zitakazokuwepo katika utekelezaji wa mradi huo na kujiletea maendeleo.
“Ni wakati sahihi sasa kuitumia fursa hii ya miradi mikubwa
ambayo inalenga kunufaisha wananchi kwa kuzingatia kuwa ajira zitazalishwa kwa
wazawa hivyo mjiandaae kikamilifu katika kuupokea mradi huu,” alieleza Mhagama.
Waziri Mhagama ameongezea kuwa, Sheria ya Mafuta imeweka wazi
kwamba watanzania na kampuni za kitanzania zinatakiwa zipewe kipaumbele wakati
wa ununuzi.
Serikali inaamini kwamba Sekta binafsi ina mchango mkubwa katika
kuinua uchumi wa nchi. Hivyo ni matarajio kwamba Mkandarasi wa mradi
atazingatia matakwa ya Sheria hii na pale ambapo kampuni za kitanzania hazina
uwezo basi ziingie ubia na kampuni za nje ili kuongeza ujuzi wa uzalishaji na
utoaji wa huduma.
Amefafanua kuwa, kwa kuzingatia dhamira ya Serikali ya awamu ya
Tano kuona Watanzania wanamiliki uchumi wao, hivyo wataendelea kuwahamasisha Watanzania kushiriki
katika miradi Mikubwa ya kimkakati na katika miradi mbalimbali.
“Serikali kupitia Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchu
Kiuchumi imejipanga kuweka mazingira wezeshi kwa watanzania ikiwa ni pamoja na
kutengeneza Sera na Sheria na miongozo inayotoa kipaumbele kwa watanzania
kupata fursa za ajira, kushiriki kwa kutoa huduma, uuzaji wa bidhaa na utoaji
wa huduma kwenye miradi inayotekelezwa hapa nchini hasa katika sekta ya
uziduaji,”amesisitiza Mhagama.
Mradi wa EACOP ni moja kati ya miradi mikubwa ambao una manufaa
mengi kwa nchi yetu na kueleza kuwa, bomba hili la mafuta ghafi litakuwa na
urefu wa km 1443 kati ya hizo km 296 zitakuwa nchini Uganda na km 1147 zitakuwa
Tanzania. Hii ni fursa kubwa kwa watanzania kwa kuwa 80% ya mradi huu utapita
Tanzania.
Aidha alibainisha mikoa itakayopitiwa na mradi huo ikiwemo
Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga na
kufafanua kuwa bomba hilo litapita katika wilaya 24, Kata 134 na vijiji zaidi
ya 180 na kutoa wito kwa wananchi kujiandaa na kuhakikisha wanaandaa mazingira
wezeshi katika kushiriki fursa zitakazotokana na uwepo wa mradi huo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Bilinith Mahenge alipongeza
jitihada zinazoendelea katika kuhamasisha na kutoa elimu kwa jamii juu ya
ushiriki wa Watanzaia katika fursa ya mradi bomba la mafuta na kuahidi
kuzimamia kikamilifu ili kuhakikisha jamii inashiriki kwa uhakika.
Post A Comment: