Naibu Waziri, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Mary Mwanjelwa
akisisitiza uhifadhi mzuri wa nyaraka alipotembelea maktaba ya Idara ya
Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini Dar es Salaam na kushuhudia baadhi ya watafiti
wakipata huduma ya taarifa zitakazowawezesha kukamilisha tafiti zao.
IMEELEZWA kuwa Mradi wa Kufua Umeme wa Maji
wa Julius Nyerere katika Maporomoko ya Mto Rufiji unaojulikana kama Julius Nyerere HydroPower Project ambao
Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza kwa vitendo uliasisiwa na Baba wa Taifa,
Mwalimu Julius K. Nyerere mnamo mwaka 1975.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Mary Mwanjelwa mara baada
kufanya ziara ya kikazi Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini Dar es
Salaam na kujionea kitabu cha Tanzania News Review cha mwaka 1977 kinachoainisha
kuwa, Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere ndiye Muasisi wa mradi huo.
Dkt. Mwanjelwa amesema, Serikali ya Awamu ya Tano
inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imekuwa mstari wa mbele katika
kutekeleza masuala yenye maslahi kwa taifa yaliyoasisiwa na Baba wa Taifa,
Hayati Mwalimu Julius K. Nyerere.
“Hakika ule usemi wa zidumu fikra za Mwalimu
Nyerere umetekelezwa kwa vitendo na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Uongozi
wa Rais Magufuli katika ujenzi wa mradi huu,” amefafanua Dkt. Mwanjelwa.
Aidha, Dkt Mwanjelwa ameitaka Idara ya Kumbukumbu na
Nyaraka za Taifa kuwa na utaratibu mzuri wa kuuhabarisha umma juu ya taarifa
muhimu za kihistoria ambazo si za siri ili watanzania wajue maamuzi mbalimbali
ya kizalendo yaliyofanywa na viongozi wao kwa mustakabali wa maendeleo ya Taifa.
Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Kumbukumbu na
Nyaraka za Taifa, Firimin Msiangi amemhakikishia Dkt. Mwanjelwa kuwa Idara yake
itaendelea kutunza vizuri na kwa uadilifu mkubwa nyaraka muhimu za nchi za
kabla na baada ya uhuru kwani nyaraka hizo ni rejea muhimu katika utendaji kazi
wa Serikali.
Post A Comment: