Naibu Waziri wa Nishati, Subira
Mgalu, akizungumza na wananchi wa Kata ya Ngarenairobi, Wilaya ya Siha,
Mkoa wa Kilimanjaro alipokuwa katika ziara ya kazi, Agosti 25, 2019.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira
Mgalu akiwasha rasmi umeme katika shule ya msingi Gararagua, iliyopo
wilayani Siha, Mkoa wa Kilimanjaro akiwa katika ziara.
**************
Na Veronica Simba – Kilimanjaro
Naibu Waziri wa Nishati, Subira
Mgalu ametoa onyo kali kwa Mkandarasi Urban & Rural Engineering,
ambaye anatekeleza mradi wa umeme vijijini awamu ya tatu mkoani
Kilimanjaro, kwa kumwambia asiijaribu serikali kwa kutikisa kibiriti
kwani njiti zimejaa na kitawaka.
Alitoa onyo hilo kwa nyakati
tofauti Agosti 25, 2019 akiwa katika ziara ya kazi kwenye Wilaya za Hai
na Siha, baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi na viongozi wao
kuwa kasi ya mkandarasi huyo hairidhishi.
Akizungumza katika mkutano na
wananchi wa Hai, Naibu Waziri Mgalu alikiri mbele yao kuwa utendaji kazi
wa mkandarasi husika unasuasua na zaidi ameonesha vitendo vya utovu wa
nidhamu kwa serikali kwa kutoitikia wito alipoitwa kushiriki kwenye
ziara hiyo pasipo kutoa sababu yoyote.
Akielezea zaidi, Naibu Waziri
alisema yeye binafsi alijaribu kuwasiliana na mkandarasi huyo kwa njia
ya simu pasipo mafanikio na hata ujumbe mfupi wa maandishi aliomtumia
kumtaka apokee simu, haukujibiwa; kitendo ambacho alikiita ni dharau.
“Sasa mimi nataka nitoe salamu
kwake. Mkandarasi Urban & Rural Engineering naona unatikisa
kibiriti, unataka ujue kama kina njiti au hakina, na kama njiti zimejaa
au zina baruti. Nataka nikwambie kibiriti kimejaa, njiti zina baruti na
kitawaka.”
“Ulichokifanya ni dharau na
unatupelekea tufanye maamuzi ya kuanza mapitio; na ni kweli nathibitisha
ameshindwa kazi,” alisema Naibu Waziri.
Kufuatia hali hiyo, alimwagiza
Msimamizi wa Mradi husika kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA),
kumjulisha mkandarasi huyo kwenda Dodoma mara moja kushiriki katika
kikao kitakachofanya mapitio ya suala hilo ili ikibidi hatua za kisheria
zichukuliwe dhidi yake.
“Kama ameshindwa kazi, tutawapatia wakandarasi wengine au hata TANESCO wanaweza kumalizia kazi husika.”
Awali, Meneja wa TANESCO wa Mkoa
wa Kilimanjaro, Mhandisi Mahawa Mkaka, alimweleza Naibu Waziri kuwa,
Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu mkoani Kilimanjaro unagharimu
kiasi cha shilingi za kitanzania takribani bilioni 12.
Alisema, Mradi unahusisha ujenzi
wa kilomita 150 za msongo wa umeme wa kilovoti 33, ujenzi wa kilomita
334 za msongo wa umeme wa kilovoti 400 na ufungaji wa mashine umba
(transfoma) 132 na kwamba unatarajiwa kuunganishia umeme jumla ya wateja
3,572 katika vijiji 75 ndani ya mkoa.
Aliongeza kuwa, kwa ujumla utekelezaji wa mradi husika mkoani humo umefikia asilimia 43 hadi sasa.
Katika ziara hiyo, Naibu Waziri
aliwasha umeme katika shule za msingi za Roo na Msamadi zilizopo
wilayani Hai, pamoja na eneo la viwanda Mwangaza na shule ya msingi
Gararagua wilayani Siha. Pia, alizungumza na wananchi wa Kata ya
Ngarenairobi wilayani Siha.
Post A Comment: