Waziri Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi, wakati
wa futari ya pamoja na watoto yatima kutoka kwenye vituo sita vya kulea
watoto yatima vya jijini Dar es Salaam, iliyofanyika katika viwanja vya
Karimjee Mei 26.2019.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya watoto yatima, kwenye futari ya pamoja na watoto yatima kutoka kwenye vituo sita vya kulea watoto yatima vya jijini Dar es Salaam, iliyofanyika katika viwanja vya Karimjee Mei 26.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya watoto yatima, kwenye futari ya pamoja na watoto yatima kutoka kwenye vituo sita vya kulea watoto yatima vya jijini Dar es Salaam, iliyofanyika katika viwanja vya Karimjee Mei 26.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaonya baadhi ya
wamiliki na waendeshaji wa makao ya watoto wasiofuata taratibu za usajili wa
watoto, wanaowatumia watoto kama mitaji au kwa maslahi binafsi na wanaoendesha
makao hayo kwa minajili ya kidini na kikabila.
Amewataka pia wamiliki hao waache mara moja kuwalea
watoto hao katika maadili yasiyofaa na yasiyo ya Kitanzania na kwamba maofisa
ustawi wa jamii wahusike moja kwa moja katika usajili wa mtoto ili kuhakikisha
kuwa ni watoto wanaostahili tu kuwekwa kwenye makao ndiyo wanasajiliwa.
Alikuwa akizungumza jana usiku (Jumapili, Mei 26, 2019) kwenye Viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam
alikokuwa mgeni wa heshima wakati wa futari ya pamoja
na watoto yatima kutoka kwenye vituo sita vya kulea watoto yatima vya jijini
humo.
“Nitoe rai kwamba watu mmoja mmoja, taasisi na makao
wazingatie baadhi ya taratibu za msingi za uendeshaji wa makao kama vile mtoto
kukuzwa katika mazingira ya familia, kuzingatia misingi ya kitaifa badala ya
misingi ya tamaduni za kigeni.
“Mtoto kukuzwa kwa kuzingatia maslahi bora ya mtoto;
kuzingatia umuhimu wa kuwa na mwendelezo katika dini ya mtoto na utamuduni
wake; kutotenganisha watoto na ndugu na kuhakikisha watoto wote wanapata huduma
stahiki, kulindwa dhidi ya vitendo vya ukatili na unyanyasaji; na kutunzwa
na kuendelezwa hadi kufikia kimo cha utimilifu wao,” alisema.
Waziri Mkuu alitumia hadhara hiyo pia kutoa
maelekezo mahsusi kwa waendeshaji wa makao pamoja na wasimamizi wa sheria na
taratibu za uendeshaji wa makao ya watoto yatima.
“Afisa Ustawi wa Jamii katika eneo yanakoanzishwa
makao, ahusike moja kwa moja katika usajili wa mtoto ili kuhakikisha kuwa ni
watoto wanaostahili tu kuwekwa kwenye makao ndio wanasajiliwa.
“Taasisi na makao zihakikishe kuwa kila mtoto
anawekewa mpango maalumu wa kuondoka kwenye makao na namna ya kumuunganisha
mtoto huyo na familia yake.
“Wamiliki wa taasisi na makao, waruhusuni maafisa
ustawi wa jamii na maafisa wengine wa Serikali wafanye ukaguzi kwa mujibu wa sheria
na wekeni utaratibu wa kuandaa taarifa za kila mwezi za watoto na taarifa ya
mwaka wa fedha,” alisema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu pia alionya dhidi ya wale “wanaowabadili
watoto dini kinyume cha sheria; wanaofanya vitendo vya unyanyasaji na ukatili
dhidi ya watoto; wasiowaruhusu watendaji wa Serikali kufanya ufuatiliaji na
usimamizi; wasioandaa mpango wa kuwaunganisha watoto na familia zao na hivyo,
kusababisha watoto kukaa kwa muda mrefu kwenye makao na wale wote wanaondesha
makao bila kuwa na leseni ya uendeshaji.”
Alisema Serikali haitowafumbia macho watu wa namna
hiyo, na mara tu watakapogundulika kuanzisha au kuendesha makao bila kufuata
taratibu, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Alisema tangu mwaka 2016 hadi sasa, kuna jumla ya
watoto 24,067 wanaolelewa katika makao yaliyosajiliwa nchini yakiwemo makao 140
yanayoendeshwa na kumilikiwa na watu au taasisi binafsi. Kati yao wavulana ni
11,925 na wasichana ni 12,142.
Alisema Serikali kupitia Wizara ya Afya, Ustawi wa
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inaratibu upatikanaji wa huduma za msingi kwenye
makao kwa kushirikiana na wadau mbalimbali. Baadhi ya huduma hizo ni pamoja na
kuwezesha upatikanaji wa Bima ya Afya kwa watoto wanaoishi katika mazingira
hatarishi. “Hadi sasa, watoto 900 kutoka Dar es Salaam, Mbeya, Kilimanjaro na
Arusha wamepatiwa kadi hizo na zoezi hilo linaendelea,” alisema.
Waziri Mkuu alisema Serikali itaendelea kusimamia na
kufuatilia kwa karibu uendeshaji wa makao ya watoto sambamba na kutoa elimu
kuhusu malezi, makuzi, haki, ulinzi na usalama wa mtoto kwa mujibu wa sheria
zinazosimamia haki na ustawi wa mtoto.
Mapema, akielezea
azma ya kuandaa futari hiyo, Mkurugenzi wa Chocolate Princess na mwandaaji wa kipindi
cha televisheni maarufu cha The Mboni
Talk Show, Bi. Mboni Masimba
alisema jumla ya watoto yatima 325 walikuwa wamealikwa kushiriki futari hiyo.
Watoto hao wanatoka vituo vya Ijango Zaida Orphanage
Centre kilichopo Sinza, Alzama Orphanage Centre (Mbagala), Ashura Foundation
(Vingunguti), Madina Orphanage Centre (Tandale), Hiyari Orphanage Centre
(Mbagala) na Hisani Orphanage Centre (Mwasonga).
Futari hiyo iliandaliwa na Mboni Masimba kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Asure Yetim Vafki, United Bank of
Africa (UBA), Junaco, Mo Dewji Foundation, Lake Oil, ASAS, AZAM, Uncle K
Catering, Zurii, Simply Special Decor na State Oil na kuhudhuriwa na watu
mbalimbali wakiwamo Balozi wa Uturuki nchini, Bw. Ali Davutoğlu, Mjumbe wa Baraza
la Ulamaa Taifa, Sheikh Issa Othman, masheikh, maimamu wa misikiti na viongozi
wa taasisi zinazojihusisha na malezi ya watoto yatima.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI
MKUU,
JUMATATU, MEI 27,
2019.
Post A Comment: