Waziri
wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga akizungumza na Gilbert Houngbo, Rais wa
Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (International Fund for
Agriculture Development – IFAD walipokutana jana Tarehe 20 Mei 2019
Jijini Dodoma. (Picha Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Waziri
wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) jana Tarehe 20 Mei 2019 alikutana na
kufanya mazungumzo na Rais wa Mfuko wa Kimataifa na Maendeleo ya Kilimo
(IFAD), Gilbert Houngbo.
Katika
mazungumzo hayo Houngbo alisema mfuko huo umetenga zaidi ya sh Billion
127.3 kwa ajili ya kufadhili miradi ya kilimo nchini kwa kipindi cha
miaka mitatu kuanzia mwaka 2020.
Alimpongeza
Rais Dk John Magufuli pamoja na serikali yake kwa juhudi kubwa
alizozifanya katika kukuza uchumi ikiwemo utekelezaji wa miradi
inayofadhiliwa na mfuko huo.
Katika
mazungumzo yake na Rais Magufuli kabla ya kuzuru Jijini Dodoma Rais
huyo wa IFAD alimueleza Dkt Magufuli kuwa baada ya kutenga fedha hizo
mfuko huo unasubiri upande wa Tanzania kuainisha maeneo mahususi ya
miradi ya kilimo ambako fedha zitaelekezwa.
Kadhalika,
alieleza kuwa ana matumaini makubwa kuwa miradi hiyo itafanikiwa kwa
kuzingatia Tanzania ni nchi yenye amani na namna serikali ilivyo na
dhamira ya maendeleo.
Naye
Waziri Hasunga alimuhakikishia kuwa fedha hizo zitakazoelekezwa katika
maeneo yenye maslahi mapana ya sekta ya kilimo ikiwemo kuwezesha
matumizi ya zana za kilimo katika uzalishaji, kuzalisha mbegu bora za
mazao, kutatua changamoto za masoko ya mazao pamoja na kuboresha ufugaji
zitakuwa chachu ya kuimarisha kilimo nchini.
Mhe Hasunga alisema kuwa tayari Bajeti ya Matumizi ya kawaida yawizara ya Kilimo imepitishwa na wabunge hivyo kupitia Mpango
wa Pili wa Taifa wa Maendeleo ya Kilimo (ASDP II) umesisitizia
mapinduzi ya viwanda na umeitambua Sekta ya Kilimo kuwa muhimili imara
kwa ajili ya upatikanaji wa malighafi za viwanda.
Alisema kiasi hicho kilichotengwa na IFAD itakuwa chachu na chagizo katika kuboresha mustakabali wa kilimo.
Alisema
kupitia Miongozo hiyo ya Kitaifa, pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya
mwaka 2015 na Sera ya Kilimo ya mwaka 2013, inayotekelezwa na Wizara
kupitia Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II)
ambayo inalenga kuleta mageuzi katika Sekta ya Kilimo na kwa kutambua
umuhimu wa kuongeza mitaji, teknolojia na ubunifu, Sekta Binafsi
inashirikishwa kikamilifu katika utekelezaji wa ASDP II wakulima nchini
wataelimika kupitia mbinu bora za kilimo na uzalishaji wenye tija.
IFAD
imekuwa katika ushirikiano na serikali ya Tanzania kufuatia uhusiano
ulioanza mwaka 1978 na kudumishwa kwa maslahi ya Watanzania.
MWISHO
Post A Comment: