Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela akitoa
taarifa yake ya mwaka 2018 kwenye Mkutano Mkuu wa 24 wa Wanahisa wa
benki hiyo leo Mei 18, 2019 uliofanyika Kituo cha Kimataifa ya Mikutano,
Ukumbi wa Simba jijini Arusha. (Picha na Yusuph Mussa).
Wajumbe
wa Mkutano Mkuu wa 24 wa Wanahisa wa Benki ya CRDB. Kikao hicho
kimefanyika leo Mei 18, 2019 kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano
(AICC), Ukumbi wa Simba jijini Arusha. (Picha na Yusuph Mussa).
MKURUGENZI Mtendaji mpya wa Benki ya
CRDB Abdulmajid Nsekela amesema wamejipanga kukabiliana na ushindani kwa siku
zijazo ikiwa ni pamoja na kuwa wabunifu zaidi hasa katika kuongeza huduma kwa
njia za kielektroniki.
Akitoa taarifa ya utendaji wa benki
hiyo kwa mwaka 2018, leo Mei 18, 2019 kwenye Mkutano Mkuu wa 24 wa Wanahisa wa
Benki ya CRDB uliofanyika kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (AICC) Ukumbi
wa Simba jijini Arusha, Nsekela alisema sekta ya fedha kwa siku zijazo
itakabiliwa zaidi na kasi kubwa ya ubunifu na mabadiliko ya teknolojia.
"Sekta ya fedha kwa siku zijazo itakabiliwa zaidi na
kasi kubwa ya ubunifu na mabadiliko ya teknolojia. Sambamba na hali hiyo,
matarajio ya wateja yataendelea kuongezeka kadri ushindani unapoongezeka. Mwaka
2019, benki na kampuni zake tanzu zitaendelea kuwekeza katika kukuza biashara,
watu na bidhaa ili kuboresha huduma kwa wateja.
"Tutatumia kikamilifu ukubwa na
upeo wetu kuboresha faida wanayopata wateja wanapotumia bidhaa zetu huku
tukihakikisha kunakuwa na utamaduni imara wa kudhibiti vihatarishi na
kujielekeza kuwa na ufanisi wa hali ya juu kiutendaji. Lengo letu ni kufanya
mageuzi ya kibiashara ili kuwa benki bora kwa wateja wadogo na wakubwa kwa
kujenga kampuni yenye mtandao mpana wa huduma unaowezeshwa na ubunifu wa
kidijitali" alisema Nsekela.
Nsekela alisema wataongeza wigo wa
huduma zao ili kufikia wilaya zote nchini kabla ya mwaka 2022 kwa kusajili
mawakala wengi zaidi kila kona nchini kuendana na kauli mbiu yao isemayo 'Ulipo
Tupo', na hatimaye kuhamasisha wateja wao wote watumie njia za kidijitali
kupata huduma.
Alisema benki inatarajia kukamilisha
ujenzi wa jengo la Makao Makuu, hatua ambayo itaboresha taswira ya benki hiyo.
Pia benki na kampuni zake tanzu zinategemea kupata mafanikio zaidi mwaka huu
kutokana na kuimarika kwa hali ya uchumi na usimamizi madhubuti wa mamlaka za
usimamizi.
Nsekela pia alizungumzia mazingira
ya utendaji, ambapo mfumo wa benki ulikuwa imara, na faida na mtaji kwenye
sekta ya benki vilianza kuongezeka kutokana na usimamizi wa Benki Kuu (BoT).
Hata hivyo, sekta ya benki ilikabiliwa na changamoto kutokana na mabadiliko ya
taratibu na miongozo ya uendeshaji ambayo ilisababisha BoT kuzifungia
benki na taasisi tano za fedha kutokana na kutokuwa na mtaji wa kutosha.
Kiwango cha mtaji katika sekta ya mabenki kilikuwa asilimia 16.3 na uwiano kati
ya mikopo na amana ulikuwa asilimia 84.2 mwaka 2018.
Nsekela alisema benki ziliboresha
taratibu za usimamizi wa mikopo ili kupunguza mikopo chechefu, ambayo ilipungua
kutoka asilimia 11.9 mwaka 2017 hadi asilimia 10.4 mwaka 2018. Kuanza kutumika
kwa utaratibu mpya wa kiuhasibu (IFRS9) kulibadirisha ukadiriaji wa hasara ya
mikopo na kuongeza kiasi kinachotengwa kwa ajili ya hasara ya mikopo na
hatimaye kupunguza faida.
"Mazingira ya uendeshaji
yaliathiriwa na mabadiliko makubwa ya teknolojia na kuongezeka ushindani kutoka
kampuni za simu, Fintechs, taasisi ndogo za kifedha na taasisi za kifedha
ambazo sio benki. Hata hivyo, benki inaendelea kuwekeza katika kujenga
ushirikiano na kutafiti mitandao mbalimbali duniani ili kupata teknolojia iliyo
bora zaidi. Kuongezeka kwa ushindani kumeifanya kupitia upya taratibu za
uendeshaji na kuziboresha na kuhakikisha wateja wetu wanapata huduma kupitia
njia mbadala za kidijitali" alisema Nsekela.
Nsekela alisema Benki ya CRDB pamoja
na kampuni zake tanzu zilipata matokeo mazuri katika taarifa zao za pamoja za
kifedha zikiwa na faida baada ya kodi ya sh. bilioni 64.1 iliyopatikana mwaka
2018. Faida kwa kampuni zote za CRDB ni sh. bilioni 642.7 ikiwa ni ukuaji wa
asilimia sita (6) ikilinganishwa na mwaka 2017.
"Benki ilitumia teknolojia ya
uhakika kuboresha utendaji na kuhakikisha wateja wanapata huduma kwa
uhakika, na kulingana na mahitaji yao. Ndani ya mwaka husika, gharama za
uendeshaji zilikuwa sh. bilioni 428.9 ikiwa ni ongezeko la asilimia 7.4
ikilinganishwa na mwaka 2017. Gharama hizi ni ndogo ikilinganishwa na
ukuaji wa wastani wa miaka mitano hali ambayo imesababishwa na mikakati
iliyotekelezwa ya kudhibiti gharama na mikakati ya mageuzi ya kidijitali.
"Faida iliyopatikana kwa benki
na kampuni zake tanzu ilikuwa sawa na malengo yaliyowekwa, matokeo ambayo
yanadhihirisha ubora na mikopo, usimamizi na taratibu, kwani pengo la hasara ya
mikopo lilipungua kwa asilimia 24.8 hadi sh. bilioni 115. Jumla ya rasilimali
ilikuwa kwa asilimia 2.3 na kufikia sh. bilioni 6,035.4 na amana za wateja
zilikuwa kwa asilimia 8.4 kutoka sh. bilioni 4,687.2 hadi mwisho wa mwaka
husika" alisema Nsekela.
"Nachukua nafasi hii
kuwashukuru kwa mara nyingine wajumbe wa Bodi za Benki ya CRDB, CRDB
Microfinance Services Company Ltd, CRDB Bank Burundi SA na CRDB Insurance
Broker Limited kwa kujituma na jitihada waliyoonesha katika kuishauri
menejimenti. Benki na kampuni zake tanzu zimefaidika kwa kiwango kikubwa
kutokana na maarifa, ujuzi na weledi na wajumbe wa bodi.
"Natambua mchango wa
Menejimenti na wafanyakazi kwa kujituma na hamasa waliyoonesha mwaka mzima. Pia
napenda kuwapongeza wanahisa, wateja, Serikali, mamlaka za usimamizi na wadau
wengine kwa kutuunga mkono katika kipindi chote cha mwaka 2018" alisema
Nsekela.
MWISHO.
Post A Comment: