*Asema sh. bilioni 44 zinaandaliwa kuwalipa wengine
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na
Uratibu), Bibi Jenista Mhagama akutane na mawaziri wa sekta nyingine na
watafute namna ya kuondoa mkanganyiko uliopo kwenye vyombo vya udhibiti hapa
nchini.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana (Jumanne, Aprili 9,
2019) Bungeni jijini Dodoma, kwenye mkutano wa 15 wakati akihitimisha hoja ya
bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka
2019/2020.
Alikuwa akitoa ufafanuzi juu ya masuala
yaliyogusa vyombo vya udhibiti kama vile Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA),
Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mkemia Mkuu wa Serikali, Mamlaka nyingine za
udhibiti pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), OSHA, BRELLA na Taasisi ya
Mionzi ambayo yaligusiwa na Waheshimiwa Wabunge.
Alisema licha ya Serikali kujenga mazingira
wezeshi na rahisi ya kufanya biashara na uwekezaji, bado kumekuwepo na
malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara na wawekezaji kama walivyoeleza
Waheshimiwa Wabunge wakati wa kuchangia hoja hiyo.
“Changamoto
nyingine ambayo imeonekana kuwa kikwazo cha biashara na uwekezaji ni
muingiliano wa majukumu ya taasisi hizo. Kwa mfano, uwepo wa majukumu yenye
kufanana kwa TFDA, TBS, Mkemia Mkuu wa Serikali, Bodi ya Maziwa, Bodi ya Nyama,
Baraza la Mifugo, EWURA, SUMATRA na TANROADS ni kikwazo kikubwa katika
kurahisisha mazingira ya kufanya biashara,” alisema.
Alisema
Serikali imekuwa ikipokea malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara kuhusu mamlaka
hizi na namna ya utendaji kazi wake. Miongoni mwa kero hizo ni mchakato wa muda
mrefu wa kupata leseni za biashara; gharama za usajili wa bidhaa zinazotozwa na
TFDA; suala la viwango vya TBS; madai ya kuwepo kwa unyanyasaji unaofanywa na Mamlaka
ya Mapato (TRA) kwa kushirikiana na polisi dhidi ya wafanyabiashara.
Pia
walibainisha changamoto nyingine kuwa ni umbali wa kutoka makao makuu na
maabara za taasisi ya mionzi hadi eneo wanalofanyia kazi kama vile bandari na
viwanja vya ndege.
“Tayari nimeshatoa maelekezo na yameanza
kufanyiwa kazi na Waheshimiwa Mawaziri wa sekta husika chini ya uratibu wa
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu) kwamba wakae pamoja
kupitia sheria na mgawanyo wa majukumu wa taasisi za udhibiti ili kuondoa
mkanganyiko uliopo sasa” alisema.
Pia Waziri Mkuu amewaagiza mawaziri husika wahakikishe
kuwa wakuu wa Mamlaka ya Mapato na taasisi zake, wanatekeleza majukumu yao kwa
weledi na kuzingatia sheria bila kuwabughudhi wafanyabiashara na wawekezaji.
Wakati wa mjadala huu, wabunge 142 walichangia
hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu ambapo kati ya hao, wabunge 98 walichangia kwa
kuzungumza moja kwa moja bungeni na wabunge 44 walichangia kwa njia ya
maandishi.
Bunge
lilikubali kupitisha sh. 148,886,523,581/-
kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake kwa mwaka
2019/2020. Kati ya hizo, sh. 86,290,355,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya
kawaida na sh. 62,596,168,581/- ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Vilevile,
Bunge liliidhinisha sh. 124,182,537,600 kwa ajili ya Mfuko wa Bunge ambapo kati
ya hizo sh. 116,573,026,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh.
7,609,511,600/- ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
(mwisho)
IMETOLEWA
NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 – DODOMA,
JUMATANO, APRILI 10, 2019.
Post A Comment: