Na Emmanuel Madafa, Mbeya
MKURUGENZI wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, SSP James Kasusura,amewasimamisha kazi watendaji wa Kata 11 kwa tuhuma za kutafuna fedha za Milioni 73 za vitambulisho vya biashara kwa wajasiriamali vilivyotolewa na Rais John Pombe Magufuli.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mkurugenzi huyo amesema, March 29, 2019 ofisi hiyo iliendesha zoezi la uhakiki wa vitambulisho hivyo na kubaini kiasi cha shilingi milioni 73 kilikuwa hakijaingizwa kwenye akaunti ya halmashauri.
Amefafanua kuwa hali hiyo iliwasababishia kwenda kufanya uhakiki wa vitambulisho hivyo kwa wahusika na kubaini kwamba kiasi cha shilingi milioni 19 kilikuwa kimetafunwa na watumishi hao ambao si waadilifu.
“Utaratibu wa fedha za vitambulisho umeweka wazi kwamba vitambulisho vinapouzwa basi fedha za malipo yote yanaingizwa kwenye akaunti ya malipo ya halmashauri jambo ambalo watumishi hawa hawakulitekeleza.”Amesema Kasusura.
Mkurugenzi huyo aliwataja watumishi hao kuwa ni Clever Mamakula anadaiwa shilingi 700,000, Anjelo Mbinda shilingi milioni 1.5, Ayubu Thomos Mweikaja shilingi 980,000, Tito Mwasyoki anadaiwa shilingi 600,000, Elmani Kapinga shilingi 800,000 na Baraka Mwabuponda shiingi milioni 1.4.
Hata hivyo, alisema watumishi wote wameandikiwa barua ya kusimamishwa kazi na wamekabidhiwa polisi na kwamba aratibu za kisheria zitafuatwa kwani bado wengine wanachunguzwa.
Aidha, amesema watumishi hao wamefikishwa mikononi mwa polisi kwa ajili ya uchunguzi na endapo watabainika kukiuka agizo, sheria na taratibu za usambazaji wa vitambulisho hivyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Post A Comment: