Rais Magufuli amemtumbua na kumrudisha kituo cha kazi OCD wa Njombe alasiri hii ya leo baada sala ya toba iliyofanyika kwa kushindwa kuzuia mauaji ya watoto mkoani humo.
Akizungumza leo Aprili 10, Rais Magufuli amesema sakata la maamuzi kuhusu mauaji ya watoto mkoani humo halikutakiwa lichukue muda mrefu.
“Ndiyo maana RPC nimemtoa alishindwa kusimamia hii kazi, ninataka mambo yatendeke haraka anapotea wa kwanza mpaka wanafikia saba umekaa kimya. Ni lazima watu tuchukue hatua haiwezekani tunaleta polisi kutoka Dar es Salaam aje kusimamia hapa wewe upo haiwezekani.
“Hivi OCD wa hapa bado yupo, aondoke naye kuanzia leo siyo OCD hapa ni lazima watu tufike mahali tuwajibike, kinamama wameumia.
“Siku nyingine ataondoka mkuu wa mkoa, RAS, mkuu wa wilaya, mkurugenzi, DAS, ofisa tarafa, mwenyekiti wa kijiji wote, mpaka katibu wa CCM na wengine wote mnaondoka ili ifike mahali tuwe tunachukua hatua haraka, watani zangu Wabena na Wakinga hauwezi kutajirika kwa kuua mtoto.”
“Wakati mwingine unaua mtoto wako ni mambo ya ajabu sana nikiletewa kesi kama hizi, sijatoa adhabu ya kunyonga nikiletewa nitamuomba malaika wangu nitasaini adhabu hii.
"Mwingine unaua mpaka mtoto wa ndugu yako, maadam hii kesi ipo mahakamani sitaki kuongea sana, niwaombe viongozi wa dini muendelee kuhubiri matendo ya Mungu,” amesema na kuongeza;
“Muone aibu kwenye hili, na wa kupiga vita hili ni nyinyi wenyewe, lakini tatizo lipo kwenu saa nyingine hamtoi ushirikiano niombe kitendo kama hiki kisirudie tena, watoto badala ya kwenda shuleni wakiwa na furaha wanacheza, wanasindikizwa mtalima saa ngapi ni lazima tabia hii tuiache.”
Baada ya hotuba hiyo Rais alimuomba kiongozi wa dini kuongoza sala ya toba kuhusu mauaji hayo yaliyotokea mwanzoni mwa mwaka huu mkoani humo.
“Kwa hii sala OCD nimemsamehe abaki hapa hapa, mwambieni kupitia maombi haya nimewasamehe, lakini nitaomba kutoa rambirambi yangu katika hizo familia nitatoa Sh5 milioni mkuu wa mkoa ataziwasilisha kwa familia hizo,” amesema.
Post A Comment: