RAIS
Dkt. John Pombe Magufuli amewataka Viongozi na Watendaji wa Wizara,
Taasisi, Wakala na Mashirika ya Umma kuvitumia vyombo vya ulinzi na
usalama ikiwemo Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Jeshi
la Kujenga Taifa (JKT)katika kazi za dharura zinazohitaji kasi ya
haraka ya utekelezaji ili kuwaletea Maendeleo Watanzania.
Akizungumza
katika hafla ya uzinduzi wa Kiwanda cha Kuchakata Mahindi katika Kambi
ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Mlale Mkoani Ruvuma leo Jumatatu (April
8, 2019), Rais Magufuli alisema JTWZ na JKT ni miongoni mwa majeshi ya
vyombo vya ulinzi na usalama yanayofanya kazi zake kwa kasi kubwa katika
miradi mbalimbali pindi wanapopewa dhamana na Serikali.
Aliongeza
kuwa pamoja na majukumu yake ya msingi katika kusimamia masuala ya
ulinzi na usalama, vyombo vya ulinzi Jeshi la Wananchi wa Tanzania
(JTWZ) wakati wa hali ya usalama majeshi hayo yamekuwa yakitumika katika
kutekeleza kazi za dharura pindi zinapotokea.
“Nawagiza
Watendaji na Viongozi wa Wizara, Taasisi za Umma ndani ya Serikali
kuvitumia vyema vyombo vyetu vya ulinzi na usalama ikiwemo majeshi yetu
ya JWTZ na JKT katika kutekeleza kazi za dharura zinatokea mara kwa
mara, kwa mfano nimwemwagiza CDF sasa aunde magari ya zimamoto na
kuyapeleka katika viwanja vyetu vya ndege ambapo ni miaka miwili sasa
pamoja na zabuni yake kutangazwa na pesa kuwepo hakuna gari hiyo pale
TAA (Mamlaka ya Viwanja vya Ndege)” alisema Rais Magufuli.
Akitolea
mfano Rais Magufuli alisema kutokana na imani kubwa ya utendaji kazi wa
JWTZ na JKT, Serikali imekuwa ikitoa zabuni za miradi mbalimbali
ikiwemo ujenzi wa nyumba na Ofisi za Serikali katika Miji ya Dar es
Salaam, Dodoma na maeneo mengine ya nchi ambapo majeshi hayo yameweza
kutekeleza miradi hiyo kwa ufanisi wa hali ya juu.
Akifafanua
zaidi Rais Magufuli alisema Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea
kuyawezesha majeshi yote ya vikosi vya ulinzi na usalama nchini ili
yaweze kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa viwanda, ambapo
alipongeza juhudi kubwa zinazofanywa na JWTZ katika kuunga mkono sera ya
Serikali ya ujenzi wa viwanda kwa kuanzisha kiwanda cha kuzalisha maji
na kiwanda cha kuchakata mahindi.
Aidha
Rais Magufuli alisema kuvitumia vyombo vya ulinzi na usalama katika
miradi ya dharura kutasaidia kuharakisha maendeleo kwa Watanzania, kwa
kuwa historia inaonyesha kuwa majeshi ya Tanzania ikiwemo JWTZ
hayajawahi kushindwa kazi yoyote inayopewa na Serikali huku na mfano
ujenzi wa ukuta katika machimbo ya madini ya Tanzanite eneo la Mererani,
ambalo lilijengwa kawa kipindi cha miezi 3 tu pamoja na ukubwa na ugumu
wa kazi hiyo katika eneo hilo.
Akizungumzia
kuhusu Kiwanda cha kuchakata mahindi cha Kambi ya JKT Mlale, Rais
Magufuli alisema Kiwanda hicho kilichojengwa kwa gharama ya Tsh Milioni
414.77 na kuwa na uwezo wa kusindika tani 400 za mahindi, hakina budi
kuwa msaada mkubwa kwa wakulima wa Mkoa wa Ruvuma ambao sehemu kubwa
wanajishughulisha na uzalishaji wa mahindi.
Kwa
upande wake, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Hussein
Mwinyi alisema mbali na majukumu ya ulinzi wa mipaka ya nchi na ulinzi
wa amani katika nchi zenye migogoro, Majeshi ya Ulinzi na Usalama nchini
ikiwemo JWTZ yamekuwa yakishiriki katika shughuli mbalimbali za
uzalishaji mali ikiwemo kuunga mkono sera ya Serikali ya Uchumi wa
Viwanda.
Alisema
kuwa Wizara yake imejipanga kuhakikisha kuwa inapunguza utegemezi wa
bajeti kwa kuhakikisha kuwa inashiriki kikamilifu katika shughuli za
uzalishaji mali ikiwemo kujihusisha na shughuli za kilimo na uvuvi ili
kuwezesha majeshi hayo kuwa na akiba ya kutosha ya chakula.
Aliongeza
kuwa katika mwaka 2019, Serikali imechukua jumla ya vijana 32,000
ikiwemo vijana 20,000 wa mafunzo kwa mujibu wa sheria na vijana 12,000
wa mafunzo ya kujitolea ambao wamekuwa chachu ya mabadiliko makubwa ya
kiutendaji na uzalishaji mali.
Naye
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Venance Mabeyo alisema
JWTZ inaendelea kuunga mkono sera ya Serikali ya kufikia uchumi wa
viwanda ambapo mbali na kuzindua viwanda vya maji na mahindi, Jeshi hilo
limejipanga kuongeza wigo wa uanzisha wa viwanda vingine vingi zaidi
ikiwemo viwanda vya kuchakata alizeti.
Alisema
hadi sasa Jeshi hilo limeweza kupiga hatua kubwa zaidi katika
uzalishaji wa malighafi mbalimbali za viwandani, na kuweza kutengeneza
sera za jeshi hilo na hivyo kusaidia kuokoa kiasi kikubwa cha fedha
zilizokuwa zikitumika hapo awali.
Post A Comment: