Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola ameliagiza Jeshi la Polisi kukomesha vitendo vya baadhi ya polisi wasio waaminifu wanaochafua taswira ya jeshi hilo kwa kushirikiana na wahalifu kufanikisha uhalifu wao na kuikwamisha serikali katika kuwahudumia na kuwaletea wananchi maendeleo.
Waziri Lugola ametoa agizo hilo wakati anafunga mafunzo ya awali ya miezi tisa kwa askari polisi 871 katika shule ya Polisi Tanzania iliyopo mjini Moshi mkoani Kilimanjaro na kwamba vitendo hivyo vinarudisha nyuma juhudi za askari wengi wanaofanya vizuri.
Akimkaribisha kufunga mafunzo hayo mkuu wa jeshi la polisi Simon Siro amewapa mwezi mmoja wa kuendelea na masomo kwa wanafunzi 22 waliofanya vibaya katika matokeo ya mitihani yao ya mwisho na atakayeshindwa baada ya hapo warudishwe makwao.
Katika taarifa yake Mkuu wa shule hiyo Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Ramadhani Mungi amesema, wanafunzi wasichana 104 walioanza mafunzo katika chuo hicho wameweka historia kwa kumaliza salama kwa mara ya kwanza.
Post A Comment: