Na
Idara ya Habari-NEC
Mwili wa aliyekuwa Mtumishi wa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) na Mwandishi wa Habari mkongwe Bwana CLARENCE SABAYA NANYARO
umeagwa jijini Dar es salaam na nyumbani kwake Kongowe-Kibaha mkoani Pwani leo
Ijumaa tarehe 05 April, 2019.
Mwili wa marehemu umesafirishwa kwenda Kijiji cha Nkoamara
Wilaya ya Arumeru Mkoani Arusha kwa mazishi yanayotarajiwa kufanyika kesho
jumamosi April 06.
Ibada ya kumuaga Marehemu Clarence Sabaya Nanyaro aliyefariki
dunia Siku ya Jumanne April 03, mwaka huu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili
alikokuwa amelazwa kwa matibabu imefanyika mapema leo asubuhi katika kanisa la
Kilutheri lililopo Hospitalini hapo na kuhudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo
wanatasnia ya Habari.
Akiwasilisha salamu kwa niaba ya Uongozi na Wafanyakazi
wa Tume Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga Kura katika Tume ya
Taifa ya Uchaguzi Bi. Giveness Aswile amemwelezea Marehemu kuwa alikuwa
mfanyakazi aliyeitumikia taasisi yake kwa kujitoa kwa hali na mali pamoja na
kujiwekea mipango kadhaa ya kuendeleza taasisi na Taifa kwa ujumla.
Nanyaro ambaye alikuwa Kaimu Mkuu wa Sehemu ya Habari
katika Idara ya Habari ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi pia alikuwa akiendelea na
masomo ya Shahada ya Uzamivu katika Mawasiliano ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu
Augustino kampass ya Dar es salaam.
Miongoni mwa taasisi alizofanya kazi wakati wa uhai
wake ni pamoja na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Ofisi ya Makamu wa Rais,
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambako
alifanya kazi hadi mauti yalipomkuta.
Marehemu Clarence Sabaya Nanyaro ambaye alizaliwa April
01 Mwaka 1969 huko katika Kijiji cha Nkoamara Wilayani Arumeru mkoa wa Arusha
ameacha mke na watoto wanne (4).
Mwisho
Post A Comment: