Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Joelson Mpina akiwahutubia wafugaji wa kijiji cha Kimotorok wilayani Simanjiro wakati wa uzinduzi wa program ya kitaifa ya mafunzo kwa wafugaji nchi nzima. |
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Joelson Mpina akikata utepe kuashiria
uzinduzi wa
program ya kitaifa ya mafunzo kwa wafugaji nchi nzima katika kijiji cha Kimotorok wilayani Simanjiro.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Joelson Mpina akivalishwa shuka la
kimasai na mzee wa mila wa kabila la kimasai Ezekiel Lesenga kama ishara
ya kumsimika katika uongozi wa sekta ya ambapo alipewa jina la Ole
Mpina wakati wa
uzinduzi wa
program ya kitaifa ya mafunzo kwa wafugaji nchi nzima katika kijiji
cha Kimotorok wilayani Simanjiro.
Na John Mapepele
Waziri wa Mifugo na Uvuvi,
Luhaga Mpina amesema Wizara imeanza program maalum ya kitaifa ya kuwafundisha
wafugaji na wavuvi kote nchini kuhusu
sheria za mifugo na uvuvi na sheria nyingine
hatua itakayowezesha kujua haki zao na kujiepusha na migogoro baina yao na watumiaji
wengine wa ardhi kwa upande wafugaji ambapo
kwa upande wa uvuvi Wizara itawafundisha ufugaji bora wa samaki,utekelezaji wa sheria
na kanuni za uvuvi,udhibiti wa ubora wa mazao ya uvuvi na ushirika wa wavuvi
ili kuboresha maisha yao.
Akizindua mafunzo hayo
kitaifa katika Kijiji cha Kimotorok Wilayani Simanjiro mkoani Manyara, Waziri
wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Joelson Mpina alisema mafunzo kwa wafugaji yatawezesha
wafugaji kutambua namna ya kutumia fedha zitokanazo na mifugo na mazao yake kwa
kuwekeza maeneo mengine kujenga makazi bora, kusomesha watoto, kukata bima ya
mifugo na kujiwekea akiba benki.
“Leo tunaanza kuzindua
mafunzo kwa wafugaji lengo likiwa ni kuwawezesha kuzijua sheria za mifugo na
kutambua haki zao ili kujiepusha na migogoro baina yao na majirani zao wakiwemo
wakulima, wahifadhi pamoja na kuelimishwa mbinu za kisasa za namna ya kuboresha
maisha na ufugaji.” Alisisitiza Mpina
Alisema kwa pande ufugaji
sheria zitakazofundishwa kuwa ni pamoja na Sheria ya Magonjwa ya Wanyama Namba
17 ya mwaka 2003, Sheria ya Ustawi wa Wanyama namba 19 ya mwaka 2008, Sheria ya
Nyanda za Malisho na Raslimali za Chakula cha mifugo Namba 13 ya mwaka 2010
pamoja na Sheria ya Wanyama pori Namba 5 ya Mwaka 2009.
Pia wafugaji hao
watafundishwa namna ya kudhibiti magonjwa ya kimkakati 12 ambayo yanadhibitiwa
kwa njia ya chanjo ikiwemo Sotoka ya mbuzi(PPR), Homa ya mapafu ya ng’ombe(CBPP),
Ugonjwa wa miguu na Midomo(FMD), Homa ya mapafu ya Mbuzi(CCPP),Mdondo(ND)Homa
ya Bonde laUfa(RVF).
Magonjwa mengine ni Mapele
ya Ngozi (LSD) Homa kali ya Nguruwe(ASF) Ndigana Kali (ECF) Kimeta(Anthrax),
Kichaa cha Mbwa (Rabbies) na ugonjwa wa
wa kutupa mimba(brucullosis) na kuokoa vifo vingi vya mifugo vinavyosababishwa
na magonjwa hayo.
Pia wafugaji watafundishwa
matumizi sahihi ya dawa,chanjo na viuatilifu vya mifugo nchini,uzalishaji wa
mbegu bora za malisho, utunzaji wa nyanda
za malisho na machunga , ufugaji kibiashara na kuweka utaratibu wa kuvuna mifugo na kuanzisha ushirika wa wafugaji.
Hivyo Waziri Mpina aliwahimiza
wafugaji kote nchini kuchangamkia mafunzo hayo kwani ndio yatakayokuwa mkombozi
baada ya kuishi kwa zaidi ya mika 50 hivyo Serikali ya awamu ya tano chini ya
Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imedhamiria kwa dhati kuwakomboa kutoka kwenye
dhiki na dhuluma waliofanyiwa.
Pia Waziri Mpina alimwagiza
Katibu Mkuu wa Mifugo kuhakikisha anakarabati bwawa la Narakauo katika Kijiji
cha Loibosoit kwenye Wilaya ya Simanjiro katika kipindi cha miezi miwili toka
sasa ili kutatua tatizo sugu la maji kwa ajili ya kunywesha mifugo na binadamu.
Aidha alimuagiza Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Yefled Myenzi kufanya marekebisho kwa
majosho yote yaliyoharibika kabla ya Juni 30 mwaka huu.
Kwa upande wake Mwenyekiti
wa Chama cha wafugaji nchini George Bajuta aliishukuru Wizara ya Mifugo kwa
uamuzi wake wa kuanzisha mafunzo hayo kwa mara ya kwanza ambayo hayajawahi kutolewa
kwa wafugaji nchini na kwamba yatawasaidia kubadilisha maisha ya wafugaji ambao
walikuwa wakidharaulika na kufukuzwa kila mahali walipokuwa wanakwenda kwa
ajili ya shughuli za ufugaji.
Pia alimwomba Waziri Mpina kuandaa
mwongozo utakaosaidia kuondoa tabia ya baadhi ya watendaji wa Serikali kukamata
hovyo mifugo kuitesa kwa muda kwa muda mrefu huku mingine ikipotea kwa kutaifishwa.
Mafunzo ya sekta za Mifugo
na Uvuvi yataendeshwa katika Wilaya zote 185 nchini na yatawafuata wafugaji na
wavuvi kwenye maeneo yao na kwa kuanza kwa upande wa mifugo yatatolewa kwenye wilaya mbili za awali za
Simanjiro na Kaliua mkoani Tabora, ambapo kwa upande wa Sekta ya Uvuvi mafunzo ya awali yatatolewa
kwenye katika wilaya za Mafia, Bagamoyo,Mkuranga,Kigambni
na Kinondoni.
Post A Comment: